NJOMBE-Mahakama ya Wilaya ya Makete mkoani Njombe imemhukumu Benjamin Nikasi Myula (28) mkazi wa jijini Mbeya kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Shilingi 500,000.
Ni baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kupokea rushwa ya Shilingi 300,000 kutoka kwa mwananchi aliyedai kumsaidia kutatua changamoto iliyohusiana na mkopo wa Benki ya NMB.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 20, 2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Irvan Msacky katika kesi namba 18693/2026 iliyofikishwa mahakamani na Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Makete.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka TAKUKURU, Yahaya Mkongwe, aliiambia mahakama kuwa,Myula ambaye alikuwa akifanya kazi ya kudai madeni kupitia kampuni ya Hollyness and Respishers Company Limited iliyokuwa katika ubia na Benki ya NMB, alipokea Shilingi 300,000 kutoka kwa mwananchi mmoja wa Kijiji cha Ng’onde, Kata ya Mlondw wilayani Makete.
Kwa mujibu wa mashtaka, mshitakiwa huyo alidai kuwa angeweza kumsaidia mwananchi huyo ili asisumbuliwe na benki kuhusu mkopo aliokuwa ameuchukua.
Mahakama ilielezwa kuwa, Myula alikuwa amepewa orodha ya watu watatu aliopaswa kuwafuatilia kwa ajili ya ukusanyaji wa madeni, lakini badala yake alikwenda kwa mlalamikaji ambaye kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa mahakamani, muda wake wa kudaiwa ulikuwa bado haujafika.
Ilidaiwa kuwa, alipofika kwa mlalamikaji huyo, Myula alifunga nyumba mbili zinazomilikiwa na familia hiyo na kuweka maandishi yanayoonesha kuwa nyumba hizo zilikuwa zinauzwa.
Kitendo hicho kilisababisha madhara kwa familia hiyo, baada ya nyumba moja kati ya hizo, ambayo ilikuwa ikiishi mama mzazi wa mlalamikaji mwenye umri wa miaka 80, kufungwa na kumlazimu mzee huyo kulala nje.
Baada ya tukio hilo, mlalamikaji alitoa taarifa kwa TAKUKURU Wilaya ya Makete, ambayo iliandaa mtego uliowezesha kukamatwa kwa Myula wakati akipokea Shilingi 300,000 zilizokuwa sehemu ya fedha za mtego.
Katika hatua za awali za kesi hiyo, Myula alikiri kosa hilo, ambalo lilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 20, 2026. Baada ya kusikiliza maelezo ya shauri hilo, Hakimu Msacky alimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya Shilingi 500,000.
Mbali na adhabu hiyo, mahakama pia iliamuru fedha hizo Shilingi 300,000 alizopokea kama rushwa zirudishwe kwa TAKUKURU, kwa kuwa zilitumika katika operesheni ya mtego iliyowezesha kukamatwa kwake.
Myula alilipa faini hiyo ya Shilingi 500,000 pamoja na kurejesha Shilingi 300,000 kwa TAKUKURU, hatua iliyomwezesha kuachiwa huru baada ya kutimiza masharti yote ya hukumu.
Kesi hiyo imekuja siku chache baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila kuzindua ofisi za kisasa za TAKUKURU Wilaya ya Makete Agosti 4, 2026, ambapo aliwataka wananchi kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa.
Aidha, kesi hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa matokeo ya wito huo kwa wananchi kushirikiana na TAKUKURU katika kuzuia na kupambana na rushwa, kwa kutoa taarifa zinazowezesha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa vitendo hivyo.
