TAKUKURU KAZINI:Raia wa Romania akamatwa kwa tuhuma za kuiba fedha benki jijini Arusha

ARUSHA-Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha inamshikilia raia wa Romania, Constantin Catalin Podoleanu, mwenye umri wa miaka 39, kwa tuhuma za kutumia taarifa za kadi za benki zilizoibwa na kujipatia fedha kwa njia haramu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema mtuhumiwa alikamatwa na maafisa wa taasisi hiyo katika eneo la Njiro jijini Arusha.

Amesema wakati wa upekuzi katika makazi ya mtuhumiwa, maafisa walibaini stakabadhi za malipo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 171, zaidi ya dola za Marekani 55,000, fedha taslimu zaidi ya Sh milioni mbili, noti za Euro 20 pamoja na Riyal 15.

Aidha, Ngailo amesema mtuhumiwa alikutwa na mashine sita za POS, kadi za benki za taasisi mbalimbali, vifaa na kemikali zinazodaiwa kutumika kutengeneza kadi bandia zinazotumika kuiba fedha kwenye akaunti za wateja wa benki.
Amesema pia mtuhumiwa alikutwa na kompyuta mpakato mbili, ambazo zinadaiwa kuwa sehemu ya vifaa anavyotumia katika shughuli hizo za wizi.

TAKUKURU imesema inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo, huku hatua zaidi za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here