Makamu wa Rais mbaroni kwa tuhuma za usafirishaji wa dawa za kulevya

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA nchini Liberia zimemkamata na kumfungulia mashtaka aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Jewel Howard-Taylor katika uchunguzi unaoendelea kuhusu mtandao wa kimataifa unaodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Taarifa hiyo imethibitishwa na Wizara ya Sheria ya Liberia, huku mamlaka zikisisitiza kuwa uchunguzi huo unalenga kubaini kwa kina mtandao na wahusika wanaodaiwa kuendesha shughuli za usafirishaji wa dawa hizo kwa njia za kimataifa.

Howard-Taylor ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais George Weah kuanzia mwaka 2018 hadi 2024, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts alipokuwa akijaribu kusafiri nje ya nchi.

Baada ya kukamatwa, alipelekwa katika makao makuu ya polisi jijini Monrovia ambako anaendelea kushikiliwa wakati taratibu za kisheria zikiendelea.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Howard-Taylor anakabiliwa na tuhuma kadhaa nzito, zikiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya, utakatishaji wa fedha, uingizaji wa dawa au kemikali zinazodhibitiwa bila kibali, kushawishi kutendwa kwa uhalifu na kula njama ya kutenda uhalifu.

Mawakili wake wamethibitisha kuwa bado yuko chini ya ulinzi wa polisi akisubiri hatua rasmi za kisheria. Wakili wake, Kabineh Ja’neh, amesema,mteja wake anaendelea kushikiliwa na mamlaka.

Wageni watatu nao watajwa

Katika hatua nyingine ya uchunguzi huo, waendesha mashtaka wa Liberia wamewafungulia mashtaka kwa kutokuwepo nchini humo raia watatu wa kigeni wanaodaiwa kuhusika na mtandao huo.

Watuhumiwa hao wanatajwa kuwa raia wawili wa Croatia na raia mmoja wa Ukraine. Mamlaka za Liberia zimesema zitashirikiana na taasisi za kimataifa za sheria na vyombo vya usalama vya nchi nyingine katika jitihada za kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Kesi hiyo imevuta hisia kubwa kutokana na nafasi ya kisiasa aliyowahi kushikilia Howard-Taylor ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wakuu katika serikali ya Weah kwa kipindi cha miaka sita.

Aidha,kukamatwa kwa Howard-Taylor kunafuatia operesheni kubwa ya vyombo vya dola nchini Liberia iliyofanyika mwezi uliopita, ambapo mamlaka zilikamata shehena kubwa ya Cocaine iliyodaiwa kuelekezwa barani Ulaya.

Operesheni hiyo imeongeza uangalizi wa kimataifa kuhusu nafasi ya Afrika Magharibi katika biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya, hususan matumizi ya eneo hilo kama njia ya kupitishia dawa zinazotoka sehemu mbalimbali kuelekea masoko ya Ulaya.

Kwa miaka kadhaa, nchi za Afrika Magharibi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya inayotumia eneo hilo kama njia ya usafirishaji.
Aidha,kukamatwa kwa shehena hiyo kubwa nchini Liberia kumeongeza shinikizo kwa mamlaka kuimarisha uchunguzi na ushirikiano wa kimataifa dhidi ya magenge ya dawa za kulevya.

Wizara ya Sheria ya Liberia imesema, haitaruhusu hadhi, mamlaka au ushawishi wa kisiasa wa mtu yeyote kuathiri mchakato wa haki katika kesi hiyo.

Pia,wizara hiyo imesisitiza kuwa itahakikisha uchunguzi na mashtaka yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria, bila upendeleo wala kuwalinda watu wenye ushawishi.

Serikali imeahidi kwamba katika kushughulikia kesi hiyo hakutakuwa na “haki ya kuchagua, ulinzi wa kisiasa, watu wasioguswa wala maelewano na uhalifu uliopangwa.”

Kauli hiyo imekuja wakati mamlaka zikikabiliwa na jukumu la kuthibitisha madai dhidi ya watuhumiwa mahakamani, huku kanuni ya msingi ya sheria ikimtaka kila mshtakiwa kuchukuliwa kuwa hana hatia hadi pale atakapothibitishwa kuwa na hatia kwa mujibu wa sheria.

Vilevile, uchunguzi huo unaendelea, na hatua zaidi za kisheria zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliopo Liberia pamoja na wale waliotajwa, lakini bado hawajakamatwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here