NA DIRAMAKINI
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi amemtembelea na kumjulia hali msanii maarufu wa muziki nchini, Zuhura Othman Soud maarufu Zuchu, kufuatia kujifungua mtoto wake salama.
Mama Mariam amefanya ziara hiyo leo Agosti 3, 2026 katika Hospitali ya Saifee iliyopo Ada Estate, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambako Zuchu amekuwa akipatiwa huduma baada ya kujifungua mtoto huyo Agosti 1, 2026.
Katika ziara hiyo, Mama Mariam amempongeza Zuchu kwa kujifungua salama na kumtakia yeye pamoja na mtoto wake afya njema, maisha marefu yenye baraka na mafanikio.
Aidha, amewatakia Zuchu na mzazi mwenzake, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, pamoja na familia yao, kheri na furaha katika hatua hiyo mpya ya maisha.
Kwa upande wao, Zuchu na Diamond wamemshukuru Mama Mariam kwa kutenga muda wake na kufika hospitalini kuwajulia hali, wakieleza kuwa ziara hiyo imekuwa faraja kubwa kwao na kwa familia katika kipindi hicho muhimu.
Ziara hiyo imeongeza salamu na pongezi kwa familia hiyo kufuatia ujio wa mtoto wao, huku ikionesha pia umuhimu wa kuwafariji na kuwapa moyo kina mama baada ya kujifungua.


