Historia ya Africa50 ni ipi, na kwa nini inaitwa Africa50?
Jibu:
Jina Africa50 linatokana na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Mwaka 2013, viongozi wa Afrika walipokutana kuadhimisha jubilei hiyo, walikubaliana kuwa kipindi cha miaka 50 kinachofuata (2013–2063) kiwe cha kuharakisha maendeleo ya bara kupitia Ajenda ya Afrika 2063 (Agenda 2063).
Ili kutekeleza maono hayo, ilibainika kuwa moja ya changamoto kubwa ilikuwa upungufu wa miundombinu na ukosefu wa mitaji ya kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Ndipo ikaasisiwa Africa50 kama taasisi maalum ya uwekezaji na maendeleo ya miundombinu yenye jukumu la kuandaa miradi inayoweza kuvutia wawekezaji (bankable projects), kuhamasisha mitaji kutoka sekta ya umma na binafsi, na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati barani Afrika.
Kwa hiyo, namba "50" inaashiria dhamira ya viongozi wa Afrika ya kuhakikisha miaka 50 ya pili ya maendeleo ya bara inakuwa ya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kupitia uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu.
2. Swali:
Africa50 Forum ni nini, na kwa nini ni muhimu kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu?
Jibu:
Africa50 Forum ni mkutano unaojumuisha Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika. Unawakutanisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wawekezaji kutoka Afrika na duniani kote kujadili namna bora ya kuharakisha uwekezaji katika miundombinu.
Kwa Tanzania, kuwa mwenyeji wa mkutano huu ni heshima kubwa na uthibitisho wa kuongezeka kwa imani ya jumuiya ya kimataifa kwa nchi yetu kama kitovu cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu katika Afrika Mashariki.
3. Swali:
Ni sababu zipi zilizoifanya Tanzania ichaguliwe kuwa mwenyeji wa Africa50 Forum 2026?
Jibu:
Tanzania imejijengea sifa ya kuwa na amani, utulivu na mazingira rafiki kwa uwekezaji. Aidha, mafanikio katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, miradi ya nishati na TEHAMA, pamoja na maboresho ya sera na mazingira ya biashara, yameifanya nchi kuwa chaguo sahihi la kuandaa mkutano huu muhimu.
4. Swali:
Mkutano huu unatarajiwa kuleta manufaa gani kwa uchumi wa Tanzania na wananchi kwa ujumla?
Jibu:
Mkutano huu unatarajiwa kuongeza uwekezaji katika miradi ya maendeleo, kufungua fursa mpya za ajira, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, kukuza biashara na kuongeza mapato ya Taifa.
Vilevile, utaongeza utalii wa mikutano (MICE) na kuitangaza Tanzania kimataifa kama nchi salama yenye mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.
5. Swali:
Ni fursa zipi za uwekezaji ambazo Tanzania itaziwasilisha kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa?
Jibu:
Tanzania itawasilisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Bandari ya Dar es Salaam, miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme, miundombinu ya TEHAMA pamoja na miradi mingine ya usafiri na uchukuzi yenye uwezo mkubwa wa kuvutia uwekezaji.
6. Swali:
Mkutano huu utachangiaje kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu barani Afrika?
Jibu:
Mkutano huu utawakutanisha watunga sera, wawekezaji, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wataalamu ili kujadili mbinu bora za kuandaa, kufadhili na kutekeleza miradi ya miundombinu. Ushirikiano huo utaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi yenye tija kwa maendeleo ya bara la Afrika.
7. Swali:
Kwa nini Africa50 inaweka msisitizo katika miradi inayoweza kuvutia uwekezaji (bankable projects), na Tanzania imejiandaaje?
Jibu:
Miradi inayoweza kuvutia uwekezaji ni ile iliyokidhi mahitaji ya kitaalamu, kisheria, kifedha na kiutawala, hivyo kuwapa wawekezaji uhakika na imani ya kuwekeza.
Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuandaa miradi inayokidhi viwango vya kimataifa ili iwe rahisi kupata mitaji kutoka kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
8. Swali:
Ni maeneo gani ya miundombinu yatakayopata kipaumbele katika mkutano huu.
Jibu:
Maeneo yatakayopata kipaumbele ni pamoja na nishati safi, miundombinu ya kidijitali na mawasiliano, usafiri na uchukuzi, pamoja na uunganishaji wa kikanda kupitia barabara, reli, bandari na njia za biashara. Pia kutajadiliwa miradi bunifu yenye uwezo wa kuigwa katika nchi mbalimbali za Afrika.
9. Swali:
Mkutano huu utaimarishaje ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi?
Jibu:
Mkutano huu utatoa jukwaa la Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha kujadiliana namna bora ya kushirikiana katika kuandaa, kufadhili na kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
10. Swali:
Serikali inatarajia matokeo gani baada ya mkutano huu?
Jibu:
Serikali inatarajia kuona ongezeko la uwekezaji katika miradi ya kimkakati, kuanzishwa kwa ushirikiano mpya kati ya Tanzania na wawekezaji wa kimataifa, pamoja na kuongezeka kwa miradi ya miundombinu itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
11. Swali:
Kwa wananchi wa Tanzania, umuhimu wa mkutano huu ni upi?
Jibu:
Wananchi watanufaika kupitia ongezeko la uwekezaji, ajira na kuboreshwa kwa huduma za miundombinu kama barabara, reli, bandari, nishati na TEHAMA. Aidha, maendeleo hayo yataongeza fursa za biashara, uzalishaji na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
12. Swali:
Mkutano huu utaisaidiaje Tanzania kujijengea nafasi kama kitovu cha biashara na uwekezaji Afrika Mashariki?
Jibu:
Kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu, Tanzania itaonesha uwezo wake wa kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa na kuwasilisha mafanikio yake katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
Hali hiyo itaongeza imani ya wawekezaji na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki na bara zima.
13. Swali:
Una ujumbe gani kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa?
Jibu:
Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji katika kutekeleza miradi ya kimkakati yenye manufaa kwa pande zote.
Nchi yetu ina mazingira ya amani na utulivu, sera zinazovutia uwekezaji, uchumi unaoendelea kukua na fursa nyingi katika sekta mbalimbali.
Tunawakaribisha wawekezaji wote kushiriki Africa50 Forum na kutumia fursa zilizopo nchini kwa manufaa yao na kwa maendeleo ya Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
