ZANZIBAR- Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto inatarajia kujenga vituo vya kutwa vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
Ni kupitia Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia (PAMOJA) unaotekelezwa na Wizara hiyo na kufadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto,Abeida Rashid Abdallah wakati akifungua kikao cha tatu cha wasimamizi wa mradi huo kilichofanyika katika ukumbi wa Mradi huo Kinazini Unguja.
Amesema,hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanawake, hususan wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi, kufanya kazi na biashara kwa utulivu huku watoto wao wakipata mazingira salama ya malezi na makuzi.
Amesema kikao hicho kimelenga kupitia na kupitisha mpango kazi pamoja na bajeti ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mradi wa PAMOJA.
Amesema mradi huo umejikita katika kuwafikia wanawake wajasiriamali waliopo kwenye vikundi, wazazi na walezi, pamoja na waathirika wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Kwa mujibu wa Abeida, maandalizi ya utekelezaji wa mradi yamefikia hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa zaidi ya miongozo 11 inayohusu ushirikishwaji wa jamii, uhifadhi wa mazingira na usalama wa wafanyakazi.
Amesema,maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo tayari yamepatikana katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, yakiwemo Pangatupu, Chwaka, Gamba, Konde na Mchanga Mdogo, Kojani, n.k.
Aidha, alisema Serikali inapanga kujenga Kituo cha Kitaifa cha Huduma za Kisaikolojia kitakachotoa huduma za ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia kwa watu wenye mahitaji ya huduma hizo.
Abeida amesema,pia Serikali kupita Mradi wa PAMOJA itajenga Nyumba Salama mbili, moja Unguja na nyingine Pemba, kwa ajili ya kutoa hifadhi na ulinzi kwa waathirika wa ukatili, udhalilishaji wa kijinsia na biashara haramu ya binadamu.
Amesema kwa ujumla, Mradi wa PAMOJA unalenga kukuza usawa wa kijinsia, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kupunguza vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, pamoja na kuimarisha malezi na makuzi ya awali ya watoto.
Amefafanua kuwa,walengwa wa mradi huo ni pamoja na wanawake wajasiriamali katika vikundi, waathirika wa ukatili na udhalilishaji, watoa huduma na wasimamizi, pamoja na wazazi na walezi wenye watoto walio chini ya umri wa miaka minne.
Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 33 za Tanzania, fedha ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka Wizara hiyo, Ali Omar Suleiman, amesema vituo hivyo vitakuwa na umuhimu mkubwa katika kuwasaidia wazazi, hasa wanawake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amesema,baadhi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za kilimo cha mwani, madagaa na biashara katika masoko hukabiliwa na changamoto ya kupata sehemu salama za kuwaacha watoto wanapokwenda kutafuta kipato.
“Lengo ni kujenga vituo vya kijamii vya kulelea watoto wadogo ili kuwasaidia akina mama wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi kuwa na mahali salama pa kuwaacha watoto wao,”amesema.
Ali amesema,vituo hivyo havitakuwa kwa ajili ya kuwahifadhi watoto pekee, bali vitatoa huduma zitakazosaidia kujenga msingi bora wa maisha yao, ikiwemo huduma za afya, lishe, ulinzi na usalama.
Amesema,mafanikio ya vituo hivyo yatategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa jamii, ambapo wananchi watahusishwa katika uendeshaji na usimamizi wa vituo hivyo kwa kushirikiana na Serikali.
Amewataka wananchi kushiriki katika kulinda na kutunza vituo hivyo ili viweze kutoa huduma endelevu na kuwahakikishia watoto mazingira salama na rafiki kwa ukuaji na maendeleo yao.
Naye Msimamizi wa Kupambana na Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kupitia Mradi huo, Nyezuma Simai Issa, alisema Serikali inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa Nyumba Salama mbili, pamoja na Kituo cha Kitaifa cha Huduma za Ushauri Nasaha na Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha mifumo ya ulinzi na huduma kwa waathirika wa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Nyezuma, taratibu za kutafuta na kupata viwanja vinavyokidhi sifa na vigezo vya Benki ya Dunia zinaendelea kukamilishwa, huku mchakato wa kumpata mshauri elekezi wa ujenzi ukiwa katika hatua za mwisho.
Amesema,mshauri huyo atakuwa na jukumu la kuandaa michoro ya majengo, nyaraka za zabuni za kumpata mkandarasi, pamoja na kusimamia na kutoa ushauri kwa Wizara katika kipindi cha utekelezaji wa ujenzi.
Nyezuma alifafanua kuwa Nyumba Salama zitakuwa maeneo maalum yenye usiri, yatakayotoa hifadhi ya muda na ya dharura kwa waathirika wa ukatili, udhalilishaji na biashara haramu ya binadamu.
Amesema lengo ni kuwaondoa waathirika katika mazingira hatarishi na kuwapatia usalama pamoja na huduma zinazohitajika wakati wa kukabiliana na changamoto walizopitia.
Aidha, amesema Mradi huo unaendelea na mchakato wa kumpata mtaalamu atakayefanya utafiti kuhusu tabia zinazochochea ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Amesema matokeo ya utafiti huo yatatumika kuandaa mwongozo wa “Bandabereho”, unaolenga kuwajengea wanandoa uelewa kuhusu malezi chanya, haki na wajibu wao, pamoja na umuhimu wa kuzuia ukatili kuanzia katika ngazi ya familia.
Nyezuma amesema timu ya wataalamu kutoka Wizara tayari ilitembelea Rwanda kwa ajili ya kujifunza namna mpango huo unavyotekelezwa, hatua inayolenga kusaidia kujenga jamii salama na inayoheshimu haki za kila mwanajamii.
Mradi wa PAMOJA unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2025 hadi 2029, ukiwa na malengo ya kukuza usawa wa kijinsia, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuimarisha malezi na makuzi ya awali ya mtoto, pamoja na kuzuia vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Mradi wa PAMOJA unatekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), katika Wilaya nane za Zanzibar.
Wilaya hizo ni Kusini, Kati, Kaskazini ‘A’ na Kaskazini ‘B’ kwa upande wa Unguja, na Chake Chake, Wete, Mkoani na Micheweni kwa upande wa Pemba.











