DODOMA-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dkt. Rahma Mahfoudh tarehe 6 Agosti 2026 ametembelea banda la Benki Kuu katika Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika jijini Dodoma, na kujionea namna wataalamu wa BoT wanavyotoa elimu na huduma mbalimbali kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mahfoudh alipata maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika banda la Benki, ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha, uwekezaji katika dhamana za Serikali, mifumo ya malipo ya taifa, usimamizi wa sekta ya fedha, utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha, fursa za ajira BoT pamoja na mafunzo yanayotolewa na Chuo cha BoT.
Vilevile, alipata maelezo kuhusu elimu inayotolewa kwa wananchi juu ya alama za usalama za noti za Tanzania na namna sahihi ya kutunza noti na sarafu ili kuhifadhi ubora na usalama wa fedha taslimu.
Akizungumza na wataalamu wa BoT katika banda hilo, Dkt. Mahfoudh aliwapongeza kwa kujituma katika kuwahudumia wananchi na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa weledi, uwazi na lugha rahisi inayoeleweka kwa makundi yote ya jamii, ili kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya Benki Kuu.
Alisisitiza kuwa, elimu ya fedha ni nguzo muhimu katika kujenga jamii yenye uelewa wa masuala ya kifedha, hivyo kuwawezesha wananchi kutumia huduma za kifedha kwa usahihi, kufanya maamuzi yenye tija, na kuchangia maendeleo endelevu ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.









