DAR-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda zimetia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya nishati inayolenga kuifanya Tanga kuwa Kituo cha Nishati cha Kikanda kwa Ukanda wa Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, nchini Tanzania iliyofanyika tarehe 5 hadi 6 Agosti 2026.
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa tarehe 6 Agosti 2026 Ikulu, jijini Dar es Salaam, kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), likiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Mussa Makame; Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC), iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bi. Proscovia Nabbanja; na Kampuni ya Vitol Bahrain, iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Tom Baker.
Hafla ya utiaji saini ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya hafla hiyo, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, alisema makubaliano hayo yana umuhimu mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uganda, huku yakifungua ukurasa mpya wa maendeleo ya sekta ya nishati katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Alieleza kuwa mradi mkubwa unaotekelezwa kupitia Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) haupaswi kutazamwa kwa thamani ya uwekezaji wake pekee, bali pia kwa manufaa yake kwa wananchi wa Tanzania, Uganda na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla wake. Miongoni mwa manufaa hayo ni kuongezeka kwa fursa za ajira, biashara, uhamishaji wa teknolojia na maarifa, ukuaji wa viwanda, maendeleo ya sekta ya usafirishaji pamoja na kuvutia uwekezaji.
“Kusainiwa kwa makubaliano haya si mwisho wa ushirikiano katika sekta ya nishati kati ya Tanzania na Uganda, bali ni mwanzo wa safari mpya ya mageuzi katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wetu,” alisema Mhe. Ndejembi.
Aidha, Waziri Ndejembi aliwapongeza na kuwashukuru Wakuu wa Nchi wa Tanzania na Uganda kwa uongozi wao madhubuti uliowezesha kufikiwa kwa hatua hiyo muhimu. Alieleza kuwa mradi wa EACOP, unaotarajiwa kugharimu takribani dola za Marekani bilioni sita, utakuwa kichocheo cha maendeleo ya sekta ya nishati na ukuaji wa uchumi katika Afrika Mashariki, Afrika ya Kati na Afrika Kusini.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhe. Dkt. Musenero Masanza, alisema Tanzania na Uganda zimeendelea kudhihirisha kwa vitendo dhamira yao ya kuendeleza mshikamano wa Bara la Afrika kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya pamoja.
“Kupitia makubaliano haya tumetoa mwelekeo na kuuthibitishia ulimwengu kuwa Afrika, kwa umoja wake, ina uwezo wa kusimamia rasilimali zake na kutekeleza miradi yake kwa manufaa ya wananchi wake,” alisema.
Mhe. Dkt. Masanza pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kutumia kikamilifu fursa zinazojitokeza katika sekta ya nishati, hatua ambayo itaongeza ufanisi, ushindani na manufaa ya kiuchumi kwa nchi zote mbili na ukanda wa Afrika Mashariki.
Tags
Bomba la Mafuta Afrika Mashariki
Dr Samia Suluhu Hassan
Foreign Tanzania
Habari
Kimataifa
Yoweri Kaguta Museveni







