NA DIRAMAKINI
MTANGAZAJI maarufu wa vipindi vya televisheni nchini Marekani, Oprah Winfrey ametangaza kuwa shule ya wasichana aliyoianzisha Afrika Kusini takribani miaka 20 iliyopita itafungwa mwishoni mwa mwaka wa masomo 2027.
Kwa mujibu wa taarifa yake, baada ya kumalizika kwa mwaka wa masomo 2027, eneo la shule hiyo kubwa ya bweni lililopo karibu na Johannesburg litakabidhiwa kwa mamlaka za elimu za eneo hilo, kama ilivyokuwa imeainishwa katika makubaliano ya awali.Shule hiyo inayojulikana kama Oprah Winfrey Leadership Academy for Girls (OWLAG), ilianzishwa kwa lengo la kutoa elimu bora kwa wasichana wenye vipaji kutoka familia na jamii zenye uwezo mdogo kiuchumi.
Winfrey amesema,wanafunzi ambao watakuwa bado hawajamaliza masomo yao wakati shule hiyo itakapofungwa watapewa ufadhili kamili wa masomo katika shule nyingineili kuhakikisha mabadiliko hayo hayaathiri maendeleo yao kielimu.
Tangu ilipoanzishwa, zaidi ya wasichana 1,000 wamehitimu katika shule hiyo huku baadhi yao wakifanikiwa kuwa madaktari, wanasheria, wahandisi, wasanii, viongozi wa kampuni na wajasiriamali.
Winfrey alianzisha mradi huo baada ya kukutana na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini na mpigania uhuru dhidi ya ubaguzi wa rangi, Nelson Mandela mwaka 2002.
Shule hiyo ilifungua milango yake mwaka 2007 katika eneo la Henley-on-Klip huko Kusini mwa Johannesburg, baada ya kujengwa kwa gharama iliyokadiriwa kufikia dola milioni 40 za Marekani.
Winfrey amesema, kufungwa kwa shule hiyo hakumaanishi mwisho wa dhamira yake ya kuwekeza katika elimu ya wasichana nchini Afrika Kusini, bali ni mabadiliko ya mfumo wa kutekeleza ndoto hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa yake, msingi unaoendesha shule hiyo unapanga kuendelea kusaidia wasichana wenye uwezo mkubwa kitaaluma kupitia mpango wa ufadhili wa masomo, utakaowawezesha kusoma katika baadhi ya shule bora nchini humo.
Winfrey mwenye umri wa miaka 72 amesema lengo lake halikuwa kujenga shule pekee, bali kuwekeza katika uwezo na mustakabali wa vijana wa kike.
Amesema, hatua hiyo mpya itaiwezesha taasisi yake kuwafikia wasichana wengi zaidi kutoka jamii mbalimbali nchini Afrika Kusini.
Pamoja na mafanikio yake, OWLAG haijakosa mijadala na changamoto tangu kuanzishwa kwake. Wakati shule hiyo ilipofunguliwa, baadhi ya wachambuzi walihoji gharama kubwa za ujenzi na anasa zilizokuwemo katika mazingira yake, ikiwamo kumbi mbili za maonesho, studio ya yoga na saluni ya urembo.
Wakosoaji walihoji iwapo fedha zilizotumika kujenga shule hiyo zingeweza kutumika kuwasaidia idadi kubwa zaidi ya wanafunzi katika maeneo mbalimbali ya Afrika Kusini.
Miezi kadhaa baada ya shule kuanza kutoa huduma, baadhi ya wanafunzi walimshutumu mfanyakazi mmoja wa zamani kwa kuwanyanyasa. Hata hivyo, mfanyakazi huyo baadaye aliachiliwa na mahakama baada ya kuondolewa mashtaka yote.Kwa sasa, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 281.
Tangazo la kufungwa kwa OWLAG pia lilizua mijadala mitandaoni kuhusu sababu za uamuzi huo, lakini mshauri wa mawasiliano anayefanya kazi na Oprah Winfrey Leadership Academy Foundation amekanusha madai kwamba shule hiyo inafungwa kutokana na usimamizi mbaya.
Bado haijafahamika ni matumizi gani yatakayotolewa kwa kampasi hiyo baada ya kukabidhiwa kwa mamlaka za elimu za eneo hilo mwishoni mwa mwaka wa masomo 2027.
Idara ya Elimu ya Mkoa wa Gauteng imesema, iko tayari kulinda na kuendeleza urithi wa shule hiyo, ikisisitiza kuwa itahakikisha taasisi hiyo inaendelea kulitumikia eneo la Gauteng huku ikiheshimu maono yaliyokuwa msingi wa kuanzishwa kwake.
Kwa upande mwingine, mafanikio ya baadhi ya wahitimu yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya urithi wa OWLAG.
Tovuti ya Oprah Daily imemnukuu Andronica Klaas, aliyehitimu mwaka 2012 na ambaye sasa ni kiongozi mwandamizi wa masuala ya uhandisi katika kampuni ya teknolojia ya Meta, akieleza kuwa shule hiyo ilimfundisha umuhimu wa maandalizi, tabia njema na kuwa na dhamira, bila kujali alikotoka.
Hivyo, licha ya kampasi hiyo kufungwa mwaka 2027, Winfrey anasisitiza kuwa dhamira ya kuwawezesha wasichana wa Afrika Kusini kupitia elimu itaendelea, huku ikitarajiwa kuwafikia vijana wengi zaidi kupitia mfumo mpya wa ufadhili wa masomo.(NA)