NA DIRAMAKINI
AKIWA na umri wa miaka 97, Kardinali Ernest Simoni amerejea katika kambi ya zamani ya gereza la kazi ngumu la Spaç nchini Albania, ambako aliwahi kufungwa na kulazimishwa kufanya kazi kwa miaka 18 chini ya utawala wa kikomunisti na kuongoza Misa ya hadhara kwa ajili ya kuwaenzi wafungwa walioteseka na kupoteza maisha katika kambi hiyo.
Misa hiyo iliyofanyika Julai 31,2026 imekuwa tukio la kihistoria lililowakutanisha waumini, viongozi wa Kanisa na wananchi mbalimbali katika eneo ambalo linatajwa kuwa moja ya alama za mateso makubwa yaliyofanywa na utawala wa kikomunisti nchini Albania.
Kambi ya Spaç, iliyojengwa mwaka 1968 karibu na mgodi wa shaba na pyrite katikati mwa Albania, ilikuwa miongoni mwa magereza yenye mazingira magumu zaidi ya kazi za kulazimishwa yaliyokuwa yakisimamiwa na serikali ya kikomunisti ya Enver Hoxha.
Simoni ambaye wakati huo alikuwa padre kijana, alitumikia sehemu kubwa ya kifungo chake katika gereza hilo.
Aliyekuwa Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, hayati Papa Francis akimsalimia Kardinali Ernest Simoni wa Albania baada ya hadhara ya kila wiki katika Ukumbi wa Paul VI, Vatican, Februari 14, 2024. Akiwa na umri wa miaka 97, Kardinali Simoni alirejea Julai 31, 2026 katika kambi ya zamani ya gereza la kazi ngumu la Spaç nchini Albania, ambako aliwahi kuongoza Misa kwa siri wakati wa miaka 18 ya kifungo chake chini ya utawala wa kikomunisti, na kuongoza Misa ya hadhara kwa kumbukumbu ya wafungwa wote walioteseka na kupoteza maisha katika kambi hiyo.Picha na VATICAN MEDIA.
Katika tukio hilo, Papa Leo XIV alituma ujumbe maalumu uliosomwa mwishoni mwa Misa, ukimpongeza Kardinali Simoni pamoja na kuwakumbuka wafungwa wengi ambao historia zao hazikuwahi kusimuliwa.
Papa alisema hakuna kifungo kinachoweza kuifunga dhamiri inayotiwa nuru na Injili, wala giza lolote linaloweza kuzuia matumaini ambayo Mungu huwaandalia watoto wake.
Aidha, aliitaja Spaç kuwa moja ya sura zenye maumivu makubwa katika historia ya Albania, akisema eneo hilo limebeba kumbukumbu za watu waliobeba mzigo mzito wa dhuluma na mateso.
Papa Leo XIV alisema, damu ya walioteseka na kufariki katika milima hiyo imeifanya ardhi hiyo kuwa shahidi wa kimya wa uaminifu, ujasiri na matumaini, huku akihoji ni sala ngapi na dua ngapi zilipaa mbinguni kutoka eneo hilo wakati wafungwa wakimtegemea Mungu kama tumaini lao la mwisho.
Kwa mujibu wa Papa, uamuzi wa Kardinali Simoni kurejea Spaç na kuongoza Misa katika eneo hilo ni ushuhuda wa dhabihu ya Kristo iliyobadilisha msalaba kutoka alama ya kifo kuwa ahadi ya uzima.
Historia ya mateso ya Kardinali Simoni ilianza mkesha wa Krismasi mwaka 1963 alipokamatwa na utawala wa kikomunisti baada ya kuongoza Misa kwa ajili ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy, aliyekuwa ameuawa.
Baada ya kifungo cha miaka 18, aliachiliwa mwaka 1981 lakini aliendelea kutambulika rasmi kama "adui wa wananchi" na kulazimishwa kufanya kazi za kuchimba na kusafisha mifereji ya maji taka hadi kuanguka kwa utawala wa kikomunisti mwaka 1990.
Licha ya mateso hayo, Kardinali Simoni aliendelea kwa siri kuwahudumia wafungwa wenzake kiroho. Aliendesha Misa kwa kukariri liturujia ya Kilatini, akasikiliza maungamo na kugawa Ekaristi kwa kutumia mikate aliyooka kwa vifaa vya kawaida na juisi ya zabibu badala ya divai.
Amesema, kila mara alipofanya huduma hizo alikuwa akiweka maisha yake hatarini kwani kama angegundulika, angehukumiwa kunyongwa mara moja.
Katika Misa ya Julai 31, Kardinali Simoni aliwaonesha waumini kofia ya chuma aliyokuwa akivaa alipokuwa akifanya kazi migodini akiwa mfungwa, ikiwa ni ishara ya mateso aliyoyapitia na ushuhuda wa imani yake.
Mwaka 2016, Papa Francis alimteua Simoni kuwa Kardinali, miaka miwili baada ya kumtembelea nchini Albania na kumtambua kama mmoja wa mashahidi hai wa uimara wa imani ya Kikristo katika kipindi cha mateso ya kidini.
Akihitimisha ujumbe wake, Papa Leo XIV alisisitiza kuwa kumbukumbu ya Spaç haipaswi kufutika pamoja na kizazi kilichopitia mateso hayo.
Alisema,anaungana katika maombi kwa ajili ya wote walioteseka na kufariki Spaç, huku akitaka historia hiyo iendelee kuwa fundisho kwa vizazi vijavyo kuhusu umuhimu wa kuheshimu utu wa kila binadamu, kuthamini uhuru na kujenga amani ya kudumu. (CNS/Vatican Media/NCR).
