Rais Dkt.Samia atoa maagizo mazito kuboresha kilimo, mifugo na uvuvi

GODFREY NNKO 

RAIS Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mbalimbali kwa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM TAMISEMI) pamoja na taasisi za utafiti, akitaka kuimarishwa kwa huduma za ugani, tafiti na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na uzalishaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Ametoa maelekezo hayo leo Agosti 8, 2026 wakati akihutubia kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt.John Samuel Malecela jijini Dodoma.

Katika hotuba yake, Rais Dkt.Samia ameelekeza kuongezwa kwa kanda za Maonesho ya Nanenane, huku akisisitiza kuwa ufungaji wa Maonesho ya Kitaifa uendelee kufanyika jijini Dodoma, lakini ufunguzi wa maonesho hayo ufanyike katika kanda nyingine.

Hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa wananchi kunufaika na elimu,maarifa, teknolojia na fursa zinazotokana na Maonesho ya Nanenane, badala ya shughuli hizo kuonekana katika eneo moja pekee.

NAESA KUPEWA MSUKUMO

Rais Samia pia amezitaka Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana kwa karibu na TAMISEMI kuhakikisha Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani za Kilimo (NAESA) unatekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi.
Ameelekeza shughuli zinazotekelezwa na NAESA kuingizwa kikamilifu katika mifumo ya mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote.

Kwa mujibu wa Rais Dkt.Samia, hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha dhana ya ugatuzi wa madaraka na kuhakikisha huduma za ugani zinawafikia wananchi wanaozihitaji, hususan wakulima, wafugaji na wadau wengine wa uzalishaji katika maeneo yao.

Pia, katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu hayo, Rais Dkt.Samia amezindua na kukabidhi magari 48 kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya NAESA.

Magari hayo yanatarajiwa kuongeza uwezo wa maafisa wa ugani kufika katika maeneo ya uzalishaji na kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
Rais ametoa wito kwa wizara, mamlaka za Serikali,Serikali za Mitaa,taasisi za umma, sekta binafsi na wadau wengine kushirikiana na NAESA ili kuhakikisha wakala huo unatimiza malengo yaliyokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwake.

TAFITI ZILENGE TEKNOLOJIA RAFIKI

Katika eneo la utafiti, Rais Dkt.Samia amezitaka taasisi zinazofanya tafiti katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kuendelea kubuni na kuendeleza tafiti zinazozingatia teknolojia za kisasa na rafiki kwa wananchi.

Amesema,tafiti hizo zinapaswa kulenga kutoa suluhisho zinazoweza kutumiwa moja kwa moja na wananchi katika kuongeza tija, uzalishaji na ufanisi wa shughuli zao za kiuchumi.

Msisitizo huo unaweka umuhimu wa kuunganisha utafiti na uzalishaji, ili maarifa yanayozalishwa na taasisi za utafiti yasiishie katika maandiko pekee, bali yafike kwa wakulima, wafugaji na wavuvi na kuleta matokeo yanayoonekana.

MIGOGORO YA WAKULIMA,WAFUGAJI

Rais Dkt.Samia pia amezitaka Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI pamoja na wadau wengine kuendelea kuchukua hatua katika kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Amesema,migogoro hiyo imepungua kwa kiasi, lakini bado kuna umuhimu wa kuendelea kuchukua hatua zaidi ili kuhakikisha makundi hayo yanaishi na kufanya shughuli zao kwa amani.
Amesisitiza kuwa, wakulima na wafugaji wote wana nafasi muhimu katika uzalishaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla, hivyo hakuna sababu ya makundi hayo kuendelea kuwa katika migogoro.

Kwa mtazamo huo, juhudi za kutatua migogoro zinahitaji ushirikiano wa Serikali, mamlaka za maeneo husika na wadau wengine ili kuhakikisha ardhi na rasilimali zinatumika kwa utaratibu unaozingatia mahitaji ya makundi yote.

MAARIFA YA NANENANE YATUMIKE KWENYE UZALISHAJI

Rais Dkt.Samia amewataka pia washiriki wa Maonesho ya Nanenane kuhakikisha maarifa, teknolojia na uzoefu wanaoupata katika maonesho hayo unafikishwa katika maeneo halisi ya uzalishaji.

Amesisitiza kuwa,elimu inayotolewa katika maonesho haipaswi kuishia katika viwanja vya maonesho, bali itumike katika mashamba, maeneo ya ufugaji, maeneo ya uvuvi, baharini na maziwa.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Rais, ni muhimu katika kuhakikisha Maonesho ya Nanenane yanakuwa sehemu ya kuchochea mabadiliko halisi katika uzalishaji na maisha ya wananchi.

Maagizo hayo yanaweka mkazo katika kuimarisha mnyororo mzima wa uzalishaji kuanzia utafiti na teknolojia, huduma za ugani, uzalishaji hadi matumizi ya maarifa katika maeneo halisi ya wananchi.
Kwa upande mwingine, kukabidhiwa kwa magari 48 kwa NAESA kunatoa nyenzo muhimu kwa utekelezaji wa huduma za ugani, huku ushirikiano kati ya wizara, Serikali za Mitaa, taasisi za umma na sekta binafsi ukitarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma hizo.

Rais Dkt.Samia amesisitiza kuwa kilimo, mifugo na uvuvi ni sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania na ustawi wa wananchi, hivyo kuimarishwa kwa huduma za kitaalamu, tafiti, teknolojia na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wazalishaji ni sehemu muhimu ya kuongeza tija na uzalishaji nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here