ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kuanzia tarehe 17 hadi 18 Agosti 2026, kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Rais Tshisekedi amewasili Zanzibar tarehe 17 Agosti 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said J. Mshana, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Akiwa nchini, Rais Tshisekedi anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na DRC, ikiwemo biashara na uwekezaji, kilimo na usalama wa chakula, madini, nishati, usafirishaji na miundombinu, afya pamoja na teknolojia ya kidijitali.
Viongozi hao pia wanatarajiwa kujadili masuala ya amani na usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu, pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuangazia pia fursa za kuendeleza ushirikiano katika maeneo yenye maslahi kwa nchi hizo mbili.
Ziara hiyo inalenga kuendeleza uhusiano wa kihistoria, kidugu na wa kimkakati kati ya Tanzania na DRC, pamoja na kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.
Aidha, ziara hiyo inatarajiwa kutoa fursa ya kujadili hatua zaidi za utekelezaji wa makubaliano na mipango mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.













