DODOMA-Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum imepiga marufuku matumizi ya watoto hususan watoto wa kiume katika sherehe na burudani zinazochochea vitendo vya mmomonyoko wa maadili na kwenda kinyume na mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka waandaaji wa sherehe na burudani za aina hiyo kujisalimisha katika kituo cha Polisi kilicho karibu nao ifikapo Agosti 19,2026 akieleza kuwa endapo hawatafanya hivyo,atamuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuwezesha Jeshi la Polisi kufanya msako mahsusi kwa kushirikiana na jamii, ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha,Waziri Gwajima amewataka Maafisa Utamaduni pamoja na Watendaji wa Serikali za Mitaa na Vijiji kuongeza umakini katika uchambuzi wa maombi ya vibali vya sherehe na burudani ili kubaini mapema viashiria vya shughuli zinazoweza kukiuka maadili na kutupilia mbali maombi yenye mashaka.
Amesema,hatua hiyo ihusishe pia sherehe zinazowahusisha watoto katika maonesho yasiyofaa, pamoja na michezo ya kuvua nguo hadharani, huku akisisitiza kuwa ukiukwaji utakapothibitika, hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.
Waziri Gwajima amewataka wananchi wenye mapenzi mema kutoa taarifa wanapobaini uwepo wa sherehe au burudani za aina hiyo, akisisitiza kuwa jukumu la kulinda maadili ya jamii na kunusuru vizazi si la Serikali pekee, bali linaanzia kwa kila mwananchi katika malezi na makuzi ya watoto.
Aidha,amewataka wananchi kukataa kutoa michango hamasa au kuwa wafuasi wa vitendo hivyo mitandaoni pamoja na kutojihusisha na sherehe zinazochochea mmomonyoko wa maadili katika jamii na Taifa kwa ujumla.
