DAR-Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, amewataka wazazi na walezi nchini kusikiliza, kutambua na kuwekeza katika vipaji vya watoto wao na kusisitiza kuwa jukumu la mzazi si kumchagulia mtoto atakachokuwa, bali kumsaidia kuwa bora katika kile anachoweza kufanya.
Amesema hayo Agosti 16, 2026 katika Mahafali ya 11 ya Darasa la Saba ya Shule ya Royal Elite, yaliyofanyika Mlimani City jijini Dar es salaam.
Mhe. Mwinjuma ameeleza kuwa kila mtoto ana uwezo au kipaji cha kipekee ambacho kinapaswa kutambuliwa na kuendelezwa ikiwa sambamba na elimu ya darasani.
"Mtoto akisema anapenda mpira, msimwambie moja kwa moja kwamba huo ni mchezo tu. Mtoto akisema anapenda kuimba, msimkatishe tamaa. Mtoto akionyesha kipaji cha sanaa, msaidieni kukiendeleza,”amesema Mhe. Mwinjuma.
Aidha, amesisitiza kuwa kulea kipaji hakumaanishi mtoto kuacha masomo, bali wazazi wanapaswa kumsaidia mtoto kuwa na elimu pamoja na kipaji, akieleza kuwa mtu anaweza kuwa msomi na wakati huo huo akawa Mwanamichezo,Msanii au Mbunifu.
Tags
Elimu
Habari
Hamis Mwinjuma
Mahafali ya Royal Elite Schools
Royal Elite Schools
Vipaji vya Watoto

















