DAR-Tanzania inazo rasilimali za maji zinazokidhi mahitaji ya nchi kwa matumizi mbalimbali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema hayo Agosti 26, 2026, katika kipindi cha Morning Trumpet kinachotangazwa na runinga ya Azam na kusisitiza Serikali inafanya kazi kuweka miundombinu ili kumfikia kila mwananchi.Amesema,Tanzania ina mita za ujazo bilioni 106 za rasilimali za maji, ikilinganishwa na mahitaji ya takribani mita za ujazo bilioni 67.
Ameainisha kuhusu hali ya upatikanaji wa maji kufika asilimia 92.5 mijini na asilimia 85.2 vijijini.
Mhandisi Waziri, amefafanua kuwa kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini, vijiji 10,758 vimefikiwa na huduma ya maji, na vijiji 1,575 bado havijafikiwa. Amesema, Serikali imejipanga kuhakikisha vijiji hivyo vinafikiwa na huduma ya maji.
Ameainisha kiwango cha upotevu wa maji nchini (NRW) kwa wastani ni asilimia 40, kinachochangiwa na uvujaji wa mabomba, uchakavu wa miundombinu, hitilafu za dira pamoja na maunganisho mapya yasiyo halali.
Amesema,Wizara ya Maji imeweka mkazo katika kuwawezesha wataalamu katika matumizi ya teknolojia na kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kupitia ushirikiano na sekta binafsi (PPP).
Mfumo wa kubaini upotevu wa maji umeanza kutumika katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam na Dodoma, kwa lengo la kubaini maeneo yenye upotevu wa maji.
