ZANZIBAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya madini, biashara, uwekezaji, miundombinu pamoja na amani na usalama.
Rais Samia amesema hayo Agosti 18, 2026, Ikulu Ndogo Zanzibar, mara baada ya kumpokea Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, akieleza kuwa nchi hizo mbili zina utajiri mkubwa wa rasilimali za madini na hivyo kuna fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu katika uchimbaji, uongezaji thamani na masoko ya madini.Amesema katika mazungumzo yao pia wamegusia masuala ya amani na usalama, ambayo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya Kanda ya Afrika na dunia kwa ujumla.
Aidha, Rais Samia amesema Tanzania, kama mshirika wa karibu wa DRC, iko tayari kuendelea kushirikiana na nchi hiyo katika kujenga uchumi unaowaunganisha wananchi wa mataifa hayo, kuongeza biashara na uwekezaji, kuboresha miundombinu na kujenga mazingira ya amani na ustawi wa pamoja.
Kuhusu miundombinu, Rais Samia amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Kalemie–Manono kutasaidia kuunganisha Tanzania na DRC, huku ikichochea shughuli za kiuchumi katika nchi hizo mbili pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ameongeza kuwa Tanzania na DRC zimesisitiza umuhimu wa kuimarisha biashara kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima, kuboresha huduma za mipakani na kuwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika fursa zitakazojitokeza.
Rais Samia amesema ziara ya Rais Félix Tshisekedi nchini Tanzania imefungua ukurasa mpya wa kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria na ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na DRC.
Tags
Dr Samia Suluhu Hassan
Félix Antoine Tshisekedi
Felix Tshisekedi
Habari
Kimataifa
Tanzania na DRC




