NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli wa mwaka 2026, ikieleza kuwa maeneo mengi yanayopata mvua za Vuli yanatarajiwa kupata mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Ladislaus Benedict Chang'a ameyasema hayo leo Agosti 18,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema,mwelekeo huo umezingatia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi husika.
Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua hizo ni pamoja na Kanda ya Ziwa Victoria inayojumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza,Shinyanga,Simiyu na Mara.
Pia,Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma hususan wilaya za Kakonko na Kibondo; Pwani ya Kaskazini, ikiwamo Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Kisiwa cha Mafia, kaskazini mwa Morogoro, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Maeneo mengine ni Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki zinazojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
TMA imeeleza kuwa,kwa kawaida msimu wa Vuli huishia mwezi Desemba, lakini mwaka huu vipindi vya mvua vinaweza kuendelea hadi Januari 2027, huku ongezeko la mvua likitarajiwa zaidi mwezi Novemba 2026.
Mvua kuanza Septemba katika baadhi ya maeneo
Dkt.Chang’a amesema, mvua za Vuli katika Kanda ya Ziwa Victoria zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026, na kuendelea hadi Januari 2027.
Katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini, mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba, huku katika Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pia zikitarajiwa kuanza katika kipindi hicho na kuendelea hadi Januari,2027.
TMA imeonya kuwa,uwepo wa El Niño unaweza kusababisha vipindi vya mvua kuanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini mapema mwezi Septemba, ingawa msimu rasmi wa Vuli katika maeneo mengi unatarajiwa kuanza Oktoba.
Aidha, hali hiyo inaweza kuchangia kuanza mapema kwa msimu wa mvua wa Novemba 2026 hadi Aprili 2027 katika baadhi ya maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.
Vilevile,TMA imeeleza kuwa, mwelekeo wa mvua umetokana kwa kiasi kikubwa na hali ya joto la bahari na mifumo mbalimbali ya anga inayotarajiwa katika kipindi cha msimu.
Joto la bahari katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuendelea kuwa Juu ya Wastani, hali inayohusishwa na uwepo wa El Niño.
Wakati huo huo, joto la bahari katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa juu zaidi ikilinganishwa na eneo la mashariki mwa bahari hiyo.
Kwa mujibu wa TMA, hali hiyo inaweza kuchochea upepo wenye unyevu kutoka baharini kuelekea maeneo ya Tanzania na hivyo kuimarisha mifumo inayosababisha mvua.
Aidha, joto la bahari la wastani hadi Juu kidogo ya Wastani linatarajiwa katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Atlantiki, karibu na pwani ya Angola.
Dkt.Chang’a amesema,kwa ujumla mifumo hiyo inatarajiwa kuimarisha hali ya mvua katika maeneo mengi ya nchini.
Pamoja na uwezekano wa mvua nzuri kunufaisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, TMA imeonya kuwa mvua za Juu ya Wastani zinaweza kuambatana na mafuriko, kutuama kwa maji na mmomonyoko wa udongo katika baadhi ya maeneo.
Katika sekta ya kilimo, unyevu uliokithiri kwenye udongo unaweza kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo. Pia kuna uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa ya mimea yanayosababishwa na kuvu, bakteria na virusi.
Amesema, miongoni mwa mazao yanayoweza kuathiriwa ni viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta,matunda na mbogamboga.
Mvua zinazoendelea kwa muda mrefu zinaweza pia kuathiri shughuli za uvunaji na kuongeza upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
Hata hivyo, TMA imesema shughuli za kilimo zinatarajiwa kuendelea kama kawaida katika baadhi ya maeneo na imewataka wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo kwa wakati, sambamba na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani.
Wakulima pia wametakiwa kutumia mbinu za kuzuia maji kutuama mashambani, kudhibiti mmomonyoko na kupunguza upotevu wa rutuba, pamoja na kuchagua mbegu na mazao yanayofaa kulingana na hali ya msimu.
Wafugaji na wavuvi watakiwa kuchukua tahadhari
Kwa upande wa mifugo, Dkt.Chang’a amesema, mvua zinazotarajiwa zinaweza kuongeza upatikanaji wa malisho na maji, hivyo kunufaisha wafugaji.
Hata hivyo, TMA imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa baadhi ya magonjwa ya mifugo, ikiwamo homa ya bonde la ufa na kuoza kwa kwato, pamoja na kuzaliana kwa wadudu wanaoweza kusambaza magonjwa.
Wafugaji wametakiwa kutumia mbinu bora za ufugaji, kutunza malisho na kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye.
Katika sekta ya uvuvi na kilimo cha mwani, TMA imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa ya mwani na kupungua kwa uzalishaji kutokana na mabadiliko ya kiwango cha chumvi baharini yanayoweza kusababishwa na maji mengi ya mvua.
Wakulima wa mwani wanashauriwa kulima katika maeneo yenye kina kirefu zaidi ili kupunguza athari za maji ya mvua yanayoingia baharini.
Wanyamapori wanaweza kuhama kutokana na mafuriko
Katika sekta ya utalii na wanyamapori, mvua zinazotarajiwa zinatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji na malisho katika hifadhi na maeneo ya wanyamapori.
Hata hivyo, mvua nyingi zinaweza kusababisha kutuama kwa maji na mafuriko, hali inayoweza kuwafanya baadhi ya wanyamapori kuhama na kuingia katika maeneo yanayozunguka hifadhi.
TMA imeonya kuwa,hali hiyo inaweza kuongeza uwezekano wa magonjwa kuenea kati ya wanyamapori na mifugo, pamoja na kuchochea migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Mamlaka husika zimetakiwa kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi na kutoa elimu kwa jamii. Wananchi nao wametakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka pale wanyamapori wanapoingia katika makazi au maeneo ya shughuli za binadamu.
Barabara, reli na bandari ziko hatarini
Dkt.Chang’a ameeleza kuwa,mvua kubwa na matukio mengine ya hali mbaya ya hewa yanaweza kuathiri miundombinu na shughuli za usafiri na usafirishaji kwa njia za barabara, reli, bandari na anga.
Miongoni mwa athari zinazoweza kujitokeza ni mmomonyoko wa udongo, kuporomoka kwa kingo za barabara, uharibifu wa madaraja na njia za reli, ikiwamo MGR na SGR, hali ambayo inaweza kuongeza hatari ya ajali na kuvuruga huduma za usafirishaji.
Katika bandari, shughuli za upakiaji na upakuaji zinaweza kuchelewa, hususan kwa mizigo inayohitaji kulindwa dhidi ya unyevu.
Wadau wa sekta ya usafirishaji wametakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu na kuchukua hatua za mapema ili kupunguza athari za mvua.
Sekta ya ujenzi nayo yaonywa
Dkt.Changa amesema,Sekta ya Ujenzi inaweza kukabiliwa na changamoto kutokana na mvua kubwa, zikiwamo kuchelewa kwa miradi, kuharibika kwa vifaa na malighafi, kuongezeka kwa gharama na kuathirika kwa ubora wa kazi.
Mvua hizo zinaweza pia kusababisha mmomonyoko wa udongo, mafuriko katika maeneo ya ujenzi na kuongezeka kwa unyevu kwenye majengo, hali inayoweza kuathiri uimara wa miundombinu.
TMA imewashauri wadau wa ujenzi kutumia utabiri huo katika kupanga utekelezaji wa miradi, kuhamisha mitambo na vifaa kutoka maeneo ya mabonde na chemchemi kabla ya mvua kuanza, na kuhifadhi vifaa vinavyoharibika kwa unyevu, kama saruji, katika maeneo salama.
Katika sekta ya nishati, maji na madini, ongezeko la kina cha maji pamoja na uchafuzi wa maziwa, mabwawa na mito linaweza kuathiri miundombinu ya maji na nishati.
Aidha, Dkt.Chang’a amesema, katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, mvua za juu ya wastani zinaweza kuongeza hatari ya maporomoko ya ardhi na kuporomoka kwa mashimo ya uchimbaji yasiyo imara.
TMA imesisitiza umuhimu wa matumizi endelevu na uhifadhi wa rasilimali za maji, huku mamlaka husika zikihimizwa kuimarisha miundombinu ya maji na nishati na kuchukua hatua za kupunguza athari za mafuriko.
Serikali za mitaa zatakiwa kujiandaa
Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetakiwa kuimarisha mifumo ya mifereji ya maji na kuhakikisha miundombinu ya kuzuia mafuriko inakuwa katika hali nzuri kabla na wakati wa msimu wa mvua.
TMA pia imezitaka mamlaka hizo kuimarisha kamati za maafa katika ngazi za vijiji na wilaya, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatua za kuchukua wakati wa mvua kubwa na mafuriko.
Hatua hizo, kwa mujibu wa TMA, zitasaidia kupunguza upotevu wa maisha, mali na uharibifu wa miundombinu.
Tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko
Sekta ya afya pia imetakiwa kujiandaa kukabiliana na uwezekano wa magonjwa ya mlipuko kutokana na maji kutuama, kutiririka na kuharibu miundombinu ya maji taka.
Dkt.Chang'a amesema, mamlaka za afya na jamii zinatakiwa kuchukua hatua za kuzuia mazalia ya mbu, kuhakikisha uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kutosha na kuandaa mipango mbadala ya kuhakikisha huduma za afya zinaendelea hata endapo miundombinu ya usafiri itaathiriwa.
Kwa upande wa sekta binafsi, mvua za kutosha zinaweza kutoa fursa kwa shughuli za kilimo na uzalishaji viwandani.
Hata hivyo, mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinaweza pia kuathiri shughuli za biashara, ujenzi, miundombinu, uhifadhi na usafirishaji wa mazao na bidhaa.
TMA imewashauri wafanyabiashara na taasisi binafsi kushirikiana na wataalamu, akiwamo TMA, ili kupata taarifa mahususi za hali ya hewa na kupanga shughuli zao kwa kuzingatia mwelekeo wa msimu.
Taasisi za benki na bima pia zimeshauriwa kuandaa huduma zinazoweza kusaidia wadau kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za hali mbaya ya hewa.
Maandalizi yaimarishwe
TMA imeonya kuwa,vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya binadamu na wanyama, kuharibu miundombinu na mali na kuvuruga huduma za kijamii na kiuchumi.
Idara ya Menejimenti ya Maafa nchini imeshauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango ya kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Sekta mbalimbali, mamlaka na kamati za usimamizi wa maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji au mitaa zimetakiwa kushirikiana katika kutoa tahadhari za mapema, elimu na miongozo kwa wananchi.
TMA yawataka wanahabari kutumia taarifa rasmi
TMA imezitaka vyombo vya habari kutumia na kusambaza taarifa rasmi za utabiri na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka hiyo pekee, ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.
Kwa mujibu wa TMA, Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 inakataza kisheria usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kutoka vyanzo visivyo rasmi.
Waandishi wa habari wametakiwa pia kutafuta mwongozo wa wataalamu wa sekta husika na kuwasilisha taarifa za hali ya hewa kwa lugha iliyo wazi na rahisi kueleweka, kwa lengo la kuongeza uelewa wa umma na kusaidia jamii kujiandaa dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.
TMA kuendelea kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa,mwelekeo uliotolewa unalenga zaidi kuonyesha mwenendo wa mvua kwa ujumla katika kipindi cha miezi mitatu na katika maeneo makubwa.
Kwa hiyo, mabadiliko ya muda mfupi na viashiria vinavyoweza kuathiri mwenendo wa mvua katika maeneo madogo yataendelea kuzingatiwa kupitia utabiri wa muda mfupi na wa kati.
TMA imewataka watumiaji wa taarifa hiyo, wakiwemo wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, wadau wa usafiri na usafirishaji, mamlaka za maji na sekta ya afya, kuendelea kufuatilia taarifa za saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka hiyo.
Aidha, TMA imesema itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho wa mwelekeo wa mvua nchini kadiri itakavyohitajika, huku wadau wakihimizwa kuwasiliana na mamlaka hiyo ili kupata utabiri mahususi unaokidhi mahitaji ya sekta zao.
Tags
Elimu ya Hali ya Hewa
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Mvua za Vuli 202
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania

