NA DIRAMAKINI
MZEE Joseph Butiku, aliyewahi kuwa msaidizi wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amesema,Tume ya Uchunguzi wa Kijinai ya Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 itasaidia kuweka wazi ukweli kuhusu matukio yaliyotokea na kutoa msingi wa hatua stahiki.
Mzee Joseph Butiku akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai ya Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Butiku ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa Tume hiyo iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na inayoongozwa na Jaji mstaafu Shabani Ally Lila.
Amesema,uwepo wa Tume hiyo ni fursa muhimu kwa Taifa kupata ukweli kuhusu yaliyotokea, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi, viongozi na makundi mbalimbali kutoa ushirikiano ili uchunguzi uweze kufanyika kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Butiku, Tanzania ina mfumo wa vyama vingi unaoruhusu kuwepo kwa upinzani, lakini tofauti za kisiasa zinapaswa kuendeshwa kwa kuheshimiana, kuaminiana na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Amesema,upinzani ni sehemu ya demokrasia, lakini unapaswa kujengwa katika mazingira ya kuheshimiana na kutumia hoja badala ya migawanyiko, akisisitiza kuwa Tume hiyo inaweza kusaidia jamii kupata taarifa na ukweli utakaowezesha kufanya maamuzi kwa uelewa mpana.
“Ningependa kushauri upinzani huu usimame kwenye heshima na kuaminiana na kiwango fulani cha ukweli. Hiki ambacho Rais anatusaidia kwa hii Tume, kujua kiwango fulani cha ukweli kitusaidie kuamua,"amesema Butiku.
Mzee Butiku amesema,Tanzania inahitaji kujenga utamaduni wa kuaminiana na kuvumiliana katika kushughulikia changamoto zinazolikabili Taifa, badala ya kila jambo kugeuzwa kuwa chanzo cha mvutano wa kisiasa.
Pia ametoa wito kwa wananchi kumheshimu Rais aliyechaguliwa na kumpa nafasi ya kutekeleza majukumu yake ya kuliongoza Taifa, huku akisisitiza kuwa wananchi wana haki ya kuzungumza na kutoa maoni yao kwa uhuru na kwa heshima.
Awasihi vijana kumuamini Rais
Akizungumza kwa msisitizo, Butiku amewataka vijana kumuamini Rais wao na kutumia fursa ya kuzungumza na viongozi kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Amesema,Rais amewahi kuwahimiza wananchi kuzungumza na kutoa maoni yao, hivyo vijana wanapaswa kutumia nafasi hiyo kwa kujenga hoja na kutoa maoni kwa heshima, huku wakizingatia misingi ya maadili ya Taifa.
“Muwe huru kuzungumza na atawasikiliza. Rais amewahi kusema, zungumzeni, muwe huru. Lakini mzungumze kwa heshima, kwa kujua kwamba nchi hii tunaheshimiana,” amesema.
Kwa mujibu wa Butiku, kuheshimiana hakupaswi kuishia katika kumheshimu Rais pekee, bali kunapaswa kuwa sehemu ya mahusiano ya wananchi kwa wananchi na viongozi kwa wananchi.
Amesema,Tanzania inapaswa kurejesha na kuimarisha misingi ya kuaminiana, kuvumiliana na kusikilizana, hasa wakati Taifa linapokabiliwa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa pamoja.
Tusipingane kwa kila kitu
Mzee Butiku amesema,tofauti za mitazamo ni jambo la kawaida katika jamii ya kidemokrasia, lakini hazipaswi kuwa sababu ya kuvunja mshikamano wa Taifa.
Ametaka wananchi na viongozi kujifunza kuongozana kwa hoja na kuheshimu mitazamo tofauti, akionya kuwa taifa haliwezi kusonga mbele iwapo kila upande utataka kupinga kila jambo bila kujenga njia ya pamoja ya kutatua changamoto.
“Lazima muanze kuaminiana na vilevile lazima muanze kuvumiliana na kusikilizana ili mpate njia ya kwenda pale ambapo mnapata matatizo,”amesema.
Amesema,Tume ya Uchunguzi wa Kijinai inaweza kuwa sehemu ya mchakato wa kulisaidia Taifa kuelewa kwa kina matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, hivyo wananchi wanapaswa kuipa nafasi na ushirikiano unaohitajika.
Vilevile amesisitiza umuhimu wa Watanzania kujenga umoja, kuaminiana na kutumia hoja katika kutatua tofauti zao, akieleza kuwa maslahi ya Taifa yanapaswa kuwa msingi wa mijadala na maamuzi yote.
Tags
Habari
jaji Mstaafu Shabani Ally Lila
Mzee Joseph Butiku
Tume ya Jaji Lila
Tume ya Uchunguzi wa Jinai
Uchaguzi Mkuu 2025