DAR-Watanzania wamehimizwa kuendelea kutunza amnani ili nchi iendelee kupokea matukio ya kimataifa ambayo yana manufaa makubwa katika ukuaji wa uchumi.
Wito huo umetolewa leo Agosti 04, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mhe. Albert Chalamila wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Mkutano Mkubwa wa wanahisa na Jukwaa la Miundombinu utakaofanyika nchini kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Agosti 05 na 06, 2026.
Amesema,mkutano huo unaotarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 1200 wakiwemo Wakuu wa Nchi, Mawaziri, wafanyabiashara na wawekezaji ni fursa muhimu kwa Tanzania kutangaza fursa za uwekezaji, hususan katika sekta ya miundombinu kupitia utekelezaji wa mfumo wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP).
Amesena kuwa, mkutano huo utakaofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kielelezo kingine cha kuimarika kwa diplomasia ya Tanzania, na ni fursa kwa Tanzania kuwasilisha na kuitangaza miradi ya maendeleo kama vile Reli ya Kisasa na Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius Nyerere kwa lengo la kuvutia uwekezaji utakaofanikisha kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050.
Amewasihi wafanyabiashara kuchangamkia fursa za mkutano huo kwa kutoa huduma bora kwa wageni zinazozingatia weledi na kuepuka kupindisha bei za bidhaa kiholela.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Setikali na Taasisi ya Africa50 unalenga kujadili mikakati ya kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu kupitia Programme for Infrastructure Development in Africa (PIDA), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Umoja wa Afrika ya Agenda 2063.
