NA DIRAMAKINI
UAMUZI wa hivi karibuni wa Serikali ya Namibia kusitisha mkataba wa dola milioni 2.4 (takriban Shilingi bilioni 6.6) na kampuni ya kiteknolojia ya Marekani ya 6th Grain Corporation, ni kengele ya heri na fundisho kubwa kwa mataifa yote ya Afrika yanayoelekea kwenye mapinduzi ya kilimo cha kidijitali.
Mkataba huo uliolenga kutumia mifumo ya Akili Unde (AI) na picha za satelaiti kufuatilia uzalishaji wa mazao, umefutwa kwa kigezo cha kutokidhi taratibu za kisheria na ununuzi wa umma.
Hata hivyo, nyuma ya pazia la kisheria, kuna somo kubwa zaidi: Utawala na Ulinzi wa Data za Chakula za Taifa (Food Data Sovereignty).
Katika karne ya 21, data ni rasilimali yenye thamani kubwa kuliko mafuta.
Tunapoingia kwenye zama za matumizi ya Akili Unde (AI) katika kilimo, taarifa zinazohusu afya ya udongo, ramani za maeneo ya uzalishaji, makadirio ya mavuno ya kila msimu, na mifumo ya hali ya hewa sio tu taarifa za kibiashara,ni taarifa nyeti za usalama wa taifa na usalama wa chakula (National Food Security).
Nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania ambayo sasa inawekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya kidijitali ya kilimo na ruzuku za mbolea, lazima ziulize swali la msingi: Je, tunapokodisha makampuni ya kigeni ya kiteknolojia kusimamia mifumo yetu, nani anamiliki data hizo? Nani anazichakata,na zinaenda kuhifadhiwa wapi?.
Kukabidhi kanzi-data (database) yote ya uzalishaji wa chakula kwa kampuni ya kigeni bila kuwepo kwa sheria kali za ulinzi wa data kunaweka mataifa yetu kwenye hatari mbili kubwa.
Mosi, ni kuongeza utegemezi wa kiteknolojia ambapo nchi inashindwa kufanya maamuzi bila idhini ya mifumo ya nje.
Pili, taarifa hizo zinaweza kutumiwa na masoko ya kimataifa au mataifa makubwa kupanga bei za mazao yetu, kudhibiti minyororo ya usambazaji, au hata kufanya maamuzi ya kijiografia (geopolitical decisions) yanayoweza kutuumiza kiuchumi kabla hata hatujavuna.
Hatua ya Namibia inapaswa kuwa kichocheo kwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) kujenga na kuwekeza kwenye miundombinu yao wenyewe ya satelaiti na mifumo ya ndani ya AI (African-owned data tech).
Ni lazima tuhakikishe kuwa makampuni ya kigeni yanapokuja, yanakuja kama washirika wa kiteknolojia wa kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa ndani, na sio wamiliki wa rasilimali zetu za kidijitali.
Serikali zetu lazima zisimame imara kuhakikisha kuwa sheria za ununuzi wa umma na sera za ulinzi wa data (Data Protection Acts) zinakuwa madhubuti kulinda wakulima wetu.
Maendeleo ya teknolojia hayapaswi kuja kwa gharama ya kuuza uhuru na usalama wetu wa chakula. Afrika lazima izalishe chakula chake, na lazima imiliki data za chakula hicho yenyewe.
Tags
DIRAMAKINI
DIRAMAKINI 24
Diramakini Blog Editorial
DIRAMAKINI NEWS 24
Habari
Makala
Maoni ya Mhariri
Tahariri DIRAMAKINI
