DAR-Zaidi ya washiriki 2,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania, pamoja na wawakilishi wa kampuni zaidi ya 50 kutoka mataifa mbalimbali duniani, wanatarajiwa kushiriki katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania (Tanzania Mining and Investment Conference – TMIC 2026), unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21 Novemba 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wenye lengo la kuendelea kuitangaza Tanzania kama eneo lenye fursa kubwa za uwekezaji katika sekta ya madini, unatarajiwa kukutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji wa kimataifa, kampuni za uchimbaji madini, taasisi za fedha, wataalamu wa teknolojia, watafiti na wadau mbalimbali katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Kupitia TMIC 2026, Tanzania inalenga kutumia jukwaa hilo kuonesha fursa zilizopo katika sekta ya madini, hususan uwekezaji katika uchimbaji wa kisasa, uchenjuaji, usafishaji wa madini, uongezaji thamani pamoja na uanzishaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za madini nchini.
Mkutano huo pia utakuwa jukwaa muhimu la kujadili namna sekta ya madini inavyoweza kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira, kukuza teknolojia, kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika shughuli za madini na kuongeza mapato ya Taifa.
Mkutano wa TMIC 2026 unatarajiwa kuwashirikisha wadau kutoka kampuni zaidi ya nchi 50 duniani, huku ukilenga kuvutia mitaji mipya na kujenga mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na wawekezaji wa kimataifa.
Sekta ya madini imeendelea kuwa moja ya nguzo muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania, ambapo Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kuongeza thamani ndani ya nchi badala ya kusafirisha madini ghafi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alisema kuwa, Tanzania itaendelea kujenga mazingira rafiki kwa uwekezaji, huku akieleza kuwa mustakabali wa sekta ya madini unaelekezwa katika kuongeza thamani ya madini, kuendeleza viwanda na kuhakikisha wananchi wanapata manufaa makubwa zaidi kupitia rasilimali zilizopo nchini.
Pia mkutano wa TMIC utakuwa na hafla ya Usiku wa Madini ambao utatoa Tuzo za kuthamini mchango wa Wadau wanaofanya vizuri kwenye mnyororo mzima wa Sekta ya Madini nchini pamoja na maonyesho ya mavazi mbalimbali na Urembo ulionakshiwa na madini.Mkutano wa TMIC 2026, unabebwa na kaulimbiu inayosema Madini yaliyoongezwa thaman chachu ya maendeleo ya viwanda na uchumi.
Tags
Anthony Mavunde
Habari
Kimataifa
Mkutano wa Madini Kimataifa
Sekta ya Madini Tanzania
TMIC 2026


