LINDI-Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kilwa, Mrakibu Msaidizi wa Polisi,ASP Adv. John Ijumba akiwa na Askari Polisi wa vyeo mbalimbali ametembelea Shule ya Msingi Nakiu iliyopo Kata ya Nanjilinji wilayani humo.
Katika ziara hiyo ametoa elimu ya ushirikishwaji jamii kwa wanafunzi hao ikiwemo kuwashauri waunde vilabu vya Polisi Jamii na Haki za mtoto ambazo zitawasaidia kutambua haki zao.
Sambamba na kujua sehemu sahihi ya kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto pindi watakapotendewa au kuviona vitendo hivyo.
ASP Adv. Ijumba aliwafundisha wanafunzi hao madhara ya kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto ni pamoja na vifo, kusababisha umasikini.
Pia,kuharibika kisaikolojia kwa waliofanyiwa vitendo hivyo, kufifisha ndoto za watoto hasa wanafunzi, ulemavu wa kudumu, magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI, ongezeko la watoto wa mitaani, kupata mtindio wa ubongo na mimba za utotoni.
Aliendelea kwa kuwataka wanafunzi kutokuwa na tamaa ya kutaka vitu vilivyopo nje ya uwezo wao badala yake waridhike na wanavyopewa na wazazi au walezi wao, kuvaa mavazi yenye stara na maadili kwenye jamii na kutokubali kupewa misaada mbalimbali ikiwemo kupakiwa kwenye vyombo vya usafiri na watu wasiowajua.
Aidha,wametakiwa kuwafanya walimu na wazazi kuwa marafiki zao wa karibu na kuweza kuwaeleza changamoto zao.
Sanjari na hayo ASP Adv. Ijumba aliwataka wanafunzi hao kuwatii na kuwaheshimu walimu wao sambamba na kuwasaidia kazi za nyumbani wazazi au walezi hasa kipindi cha likizo.
Vilevile alisisitiza kufanya kazi kwa weledi wanazopewa shuleni na walimu wao mfano kusafisha maeneo, kutunza maua, kulima bustani za mbogamboga, kuchimba mashimo ya kutupia takataka pamoja na kuzingatia masomo yao na kusema.
"Elimu sio lazima iwe ya darasani pekee, hata ukienda kulima kwenye shamba la shule ni elimu pia ambayo itawasaidia hapo baadae baada ya kumaliza masomo yenu."
