KILIMANJARO-Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wakiwa na jumla ya mita 14 walizoziiba usiku wa kuamkia Agosti 22, 2026 kwenye Mji Mdogo wa Himo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhandisi Kija Limbe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo amesema, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya hujuma hizo hususani wizi wa mita za maji.Mhandisi Limbe amesema,kutokana na hujuma hizo Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi ili kuhakikisha huduma inarejea kwa wateja wanaokuwa wamepata kadhia ya kuibiwa.
Kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Agosti,2026 amesema, mamlaka imeibiwa jumla ya mita 641 zenye thamani ya Shilingi milioni 97,175,600.
Mhandisi Limbe amelishukuru Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa kuendelea kushirikiana na mamlaka katika kuhakikisha hujuma hizo zinatokomezwa.
"Aidha, niwashukuru kwa dhati kikundi cha Ulinzi Shirikishi (Sungusungu) cha Mji Mdogo wa Himo kilichosaidia na kushirikiana na Jeshi la Polisi na kuhakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa."
Kwa sasa watuhumiwa hao wako kwenye mikono ya sheria wakisubiri taratibu za kuwapeleka mahakamani zikamilike.