MOROGORO-Wizara ya Fedha kupitia Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, imeandaa Jukwaa la Kwanza la Ufuatiliaji na Tathmini la Wizara ya Fedha kwa Mwaka 2026/2027 linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Cate Hotel, mkoani Morogoro.
Kuelekea Uzinduzi wa Jukwaa hilo, Wizara ya fedha imewakutanisha wawezeshaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Chuo Kikuu Mzumbe, Wakuu wa Idara, Vitengo na Sehemu za Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha, Maafisa Viungo wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Maafisa wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Fedha.
Jukwaa la Ufuatiliaji na Tathmini la Wizara ya Fedha, lenye Kaulimbiu “Kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini kwa Maamuzi Yenye Ushahidi” limetanguliwa na mijadala kuhusu mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji mbalimbali.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha ufuatiliaji na tathmini kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Fedha.










