WIZARA ya Fedha imeendesha kikao kazi kilicholenga kujadili andiko la mapendekezo ya kuanzishwa kwa Kampuni ya Umma ya Udhamini wa Mikopo Tanzania, itakayolenga kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali na sekta binafsi nchini.
Kikao hicho kimeongozwa na Kaimu Kamishna Msaidizi, Sehemu ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Mudith Cheyo, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo madhubuti wa udhamini wa mikopo ili kuongeza fursa za upatikanaji wa fedha kwa wajasiriamali.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Cheyo alieleza kuwa kampuni inayopendekezwa itasaidia kuimarisha huduma za udhamini wa mikopo, kupunguza vihatarishi kwa taasisi za fedha na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.
Meneja Huduma za Wakala wa Serikali, Benki Kuu Tanzania, Bw. Sadiki Nyanzowa, ameeleza kuwa Kampuni hiyo itasaidia kuongeza uaminifu na kupunguza vihatarishi katika utoaji wa mikopo, hivyo kuwezesha taasisi za fedha kuwa na mazingira bora ya kuwafikia wakopaji wengi zaidi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo madhubuti ya uendeshaji, usimamizi na uwajibikaji ili kuhakikisha Kampuni hiyo inatimiza malengo yake na kutoa mchango katika kukuza shughuli za kiuchumi nchini.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha katika Wizara ya Fedha, Bw. Kelvin Kalengela, alitoa ufafanuzi kuhusu mapendekezo ya uanzishwaji wa kampuni hiyo pamoja na majukumu yanayotarajiwa kutekelezwa.
Kwa mujibu wa andiko hilo, kampuni inayopendekezwa itatoa huduma za udhamini wa mikopo, huduma za uendelezaji wa biashara pamoja na taarifa na takwimu zitakazosaidia taasisi za fedha katika kufanya maamuzi ya utoaji wa mikopo.
Uanzishwaji wa kampuni hiyo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuchochea uwekezaji, ajira na ukuaji wa uchumi nchini.





