MWANZA-Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) ikiongozana na Menejimenti imekamilisha ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Makutopora hadi Mwanza, na kueleza kuridhishwa na hatua kubwa iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR).
Akitathmini matokeo ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC Bw. Jaffer Machano ameeleza kuwa bodi imekagua maendeleo ya ujenzi kuanzia kipande cha tatu hadi kipande cha tano na kujiridhisha kuwa kazi inakwenda kulingana na mipango iliyowekwa.
Bw. Machano amesisitiza kuwa,matarajio ni kukamilika kwa mradi huo na treni ya SGR na kuanza uendeshaji ifikapo mwishoni mwa mwaka 2028 yapo kwenye mwelekeo sahihi na yanasadifu maelekezo ya Serikali.



