NHC yarejesha tena tabasamu kwa wasioona Dar, wapewa msaada wa fimbo maalumu (white cane)

DAR-Wanachama wa vyama na vikundi vya watu wasioona jijini Dar es Salaam wamelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuendelea kuwaunga mkono katika jitihada za kuboresha maisha yao, baada ya shirika hilo kukabidhi msaada wa fimbo maalumu za kutembelea (white cane) 100 kwa vikundi viwili vya wasioona vya Ilala na Kinondoni.
Fimbo hizo zimekabidhiwa leo Septemba 3, 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa NHC wa kushirikiana na jamii na kuchangia katika kuboresha ustawi wa makundi yenye mahitaji maalumu nchini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Afisa Uhusiano wa NHC, B.Yamlihery Ndullah amesema,shirika hilo limeendelea kutekeleza sera yake ya huduma kwa jamii kwa kuhakikisha linairudishia jamii sehemu ya kile linachokipata kupitia shughuli zake.

Pia, amesema msaada huo umetolewa chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, ambapo kila kikundi kimekabidhiwa fimbo 50, kwa lengo la kuwasaidia watu wenye ulemavu wa macho katika shughuli zao za kila siku.

“Milango yetu ipo wazi. Msisite kuja NHC mnapokuwa na mahitaji, na tutawasaidia kulingana na uwezo na bajeti iliyopo kwa wakati huo,”amesema Bi.Ndullah.

VINGUNGUTI

Akizungumza kwa niaba ya Nia Njema Wasioona Group cha Vingunguti Wilaya ya Ilala, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Bw.Khalifa Mahamoud Idd amesema,msaada wa fimbo hizo ni muhimu kwa wanachama kwa kuwa utawarahisishia kutembea na kutekeleza shughuli zao za kila siku kwa usalama zaidi.
Kikundi hicho, ambacho kiko chini ya Chama cha Wasioona Wilaya ya Ilala (TLB) kinajishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Iddi amesema, pamoja na kushukuru kwa msaada huo, wanaiomba NHC pia kuwasaidia misaada itakayowawezesha kujitegemea kiuchumi.

Ametaja baadhi ya mahitaji yao kuwa ni bajaji, pikipiki, mashine za kufyatulia tofali na mashine za kukamulia juisi ambazo amesema, zinaweza kuwawezesha kuanzisha au kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara.

Amesisitiza kuwa, watu wenye ulemavu wa macho nao wana familia, majukumu na mahitaji ya kila siku kama ilivyo kwa watu wengine, hivyo wanahitaji kuwezeshwa ili waweze kujitegemea badala ya kutegemea misaada.

“Tukipewa support na nguvu tunaweza kufanya kazi na kujitegemea. Walemavu wakiwezeshwa wanaweza na hawatakuwa tegemezi,” amesema.

Aidha, Iddi ameiomba NHC kuwasaidia kupata ofisi ya kudumu, akisema kwa sasa kikundi hicho kinatumia ofisi ya kupanga na gharama za kodi zimekuwa changamoto kwao.

Kwa upande wake, mjumbe wa kikundi hicho, Shaban, aliishukuru NHC kwa msaada huo na kuomba shirika hilo liendelee kuwazingatia hata pale watakapohitaji msaada mwingine, ikiwemo fimbo mpya.
Amesema, fimbo hizo hutumika kwa muda na hatimaye kuchakaa, hivyo wanahitaji kuendelea kupata msaada ili kuhakikisha wanachama wenye uhitaji wanaendelea kuwa na vifaa hivyo muhimu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Ilala, Chalamanda Mohammed ametoa shukrani kwa NHC na kuiomba jamii na taasisi mbalimbali kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu.

Mohammed amesema,chama hicho pia kimenunua eneo lililopo Chanika, Dar es Salaam ambalo linatarajiwa kutumika kwa shughuli za ufugaji, kilimo, uzalishaji wa matofali na shughuli nyingine za ujasiriamali.

KINONDONI

Kwa upande wa Chama cha Wasioona Mkoa wa Dar es Salaam (TLB) chenye ofisi zake Kinondoni Manyanya, viongozi wa chama hicho wameeleza kuwa, msaada huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wanachama wao.

Mwenyekiti wa chama hicho, Paul Zumba akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu wa macho Mkoa wa Dar es Salaam, ameishukuru NHC kwa msaada huo na kusema fimbo hizo ni nyenzo muhimu katika maisha ya kila siku ya watu wenye ulemavu wa macho.
Amesema, fimbo hizo huwasaidia kutambulika wanapotembea katika maeneo mbalimbali, hali inayorahisisha wananchi wengine kuwasaidia wanapokuwa wanahitaji msaada.

Kwa mujibu wa Zumba, hata baadhi ya watu wenye uono mdogo hunufaika na fimbo hizo kwa sababu zinawasaidia kutembea kwa usalama na kugundua vitu au vikwazo vilivyopo mbele yao.
"Fimbo hizi zinatusaidia sana. Mtu akituona tukiwa nazo anatambua kwa urahisi kuwa tuna ulemavu wa macho na hivyo anaweza kutusaidia. Pia zinatusaidia kugundua vitu vilivyo mbele yetu na kupunguza uwezekano wa kupata ajali,”amesema.

Amesema,matumizi ya fimbo hizo yanaweza kusaidia kupunguza ajali na madhara mbalimbali yanayoweza kuwakabili watu wenye ulemavu wa macho wanapokuwa katika maeneo ya barabara au mazingira yenye vikwazo.

Zumba pia ametoa salamu za shukrani kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw.Hamad Abdallah kwa kuwa tayari kusikiliza mahitaji ya watu wenye ulemavu wa macho na kuwafungulia milango wanapofika katika shirika hilo kuomba msaada.
Amemuomba Mkurugenzi Mkuu huyo kuendelea kuwaunga mkono, si katika upatikanaji wa fimbo pekee, bali pia katika mahitaji mengine yanayoweza kuwawezesha watu wenye ulemavu wa macho kujikwamua kiuchumi na kuishi maisha ya kujitegemea.

Viongozi hao kwa pamoja wameeleza kuwa, uwezeshaji wa watu wenye ulemavu kupitia vifaa saidizi na fursa za kiuchumi ni muhimu katika kujenga jamii jumuishi, yenye kuwapa nafasi watu wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here