NA DIRAMAKINI
UBALOZI wa China nchini Somalia umepinga vikali maelezo yaliyotolewa na Ofisi ya Taiwan nchini Somaliland kuhusu hadhi ya Taiwan na tafsiri ya Beijing kuhusu Azimio Na. 2758 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lililopitishwa mwaka 1971 na kurejesha uwakilishi wa Jamhuri ya Watu wa China (PRC) katika Umoja wa Mataifa.
Mzozo huo wa kidiplomasia umeibuka baada ya Ofisi ya Taiwan mjini Hargeisa kupinga madai ya Beijing kwamba Azimio hilo linatokana na msingi wa kanuni ya China Moja, ikisema Taiwan na Jamhuri ya Watu wa China si tawala zilizo chini ya nyingine na kwamba azimio hilo halitaji Taiwan moja kwa moja.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na Ubalozi wa China nchini Somalia umesisitiza msimamo wa Beijing kwamba kuna China Moja na kwamba Taiwan ni sehemu ya eneo la China.
Beijing imetumia pia matukio ya kihistoria, ikiwemo Tamko la Cairo la mwaka 1943 na Tangazo la Potsdam la mwaka 1945, kama sehemu ya msingi wa msimamo wake kuhusu hadhi ya Taiwan.
Ubalozi huo umesema kanuni ya “China moja” ndiyo msingi wa kisiasa uliopelekea kupitishwa kwa Azimio Na. 2758 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa Oktoba 25, 1971.
Azimio hilo lilirejesha haki za Jamhuri ya Watu wa China katika Umoja wa Mataifa na kuitambua Serikali yake kama wawakilishi pekee halali wa China katika Umoja wa Mataifa, huku wawakilishi wa Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Chiang Kai-shek wakiondolewa.
Hata hivyo, maandishi ya azimio hilo hayatumii moja kwa moja neno Taiwan, jambo ambalo Taiwan imekuwa ikilitumia kupinga tafsiri ya Beijing kwamba azimio hilo linathibitisha msimamo wake kuhusu hadhi ya Taiwan.
Kwa upande wake, Beijing inasisitiza kuwa azimio hilo lilitatua suala la nani anaiwakilisha China katika Umoja wa Mataifa na kwamba halipaswi kutafsiriwa kwa namna inayoruhusu Taiwan kuwa na uwakilishi tofauti wa kimataifa kama nchi inayojitegemea.
“Kanuni ya China Moja ndiyo sharti na msingi wa kisiasa wa Azimio Na. 2758 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,” ubalozi huo umesema, ukiongeza kuwa azimio hilo haliwezi kutumiwa kuhalalisha dhana ya kuwepo kwa china mbili au china moja, taiwan moja.
China pia imedai kuwa,nyaraka rasmi za Umoja wa Mataifa zilizotolewa baada ya kupitishwa kwa azimio hilo zimekuwa zikirejea Taiwan kwa jina la "Taiwan, Province of China”, jambo ambalo Beijing inaliona kama ushahidi unaoendana na msimamo wake.
Hata hivyo, suala la hadhi ya Taiwan limeendelea kuwa miongoni mwa masuala nyeti zaidi katika siasa za kimataifa, huku pande hizo zikiwa na tafsiri tofauti kuhusu uhusiano wa Taiwan na Jamhuri ya Watu wa China.
Taiwan ina serikali yake, jeshi na mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia na rasmi hutumia jina la Jamhuri ya China (Republic of China).
Beijing, kwa upande wake, inaitambua Taiwan kama sehemu ya China na imekuwa ikipinga juhudi za Taiwan kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na nchi nyingine au kushiriki kama chombo tofauti katika mashirika ya kimataifa.
Mzozo huo pia una uhusiano na mahusiano yanayoendelea kati ya Taiwan na Somaliland, eneo linalojitawala kaskazini mwa Somalia.
Taiwan na Somaliland zilianzisha ofisi za uwakilishi katika miji mikuu ya pande hizo mwaka 2020, hatua iliyofungua njia ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali, yakiwamo afya, kilimo, teknolojia na elimu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Taiwan bado inaitambua ofisi yake mjini Hargeisa kama Taiwan Representative Office in the Republic of Somaliland.
Hatua hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na Beijing, ambayo inatambua mamlaka ya Somalia juu ya Somaliland na imekuwa ikipinga uhusiano rasmi kati ya Taiwan na Somaliland.
Taarifa ya Ubalozi wa China imekuja siku tatu baada ya Beijing kumkosoa Rais wa Somaliland, Abdirahman Mohamed Abdullahi Irro, kufuatia kauli alizotoa kuhusu Taiwan wakati wa ziara yake nchini Marekani.

China imesema kauli hizo zinakiuka kanuni ya China Moja na wakati huo huo ikasisitiza kuunga mkono umoja na mamlaka ya eneo la Somalia ikiwemo Somaliland.
Somaliland ilijitangazia kujitawala na kujitenga na Somalia mwaka 1991 na tangu wakati huo imeendesha taasisi zake za kisiasa na kiutawala kwa kiwango kikubwa, ingawa bado haijatambuliwa kwa upana kimataifa kama nchi huru.
Aidha,kwa upande wa Beijing, Somalia ndiyo nchi yenye mamlaka ya kisheria juu ya Somaliland, msimamo unaoendana na sera ya China ya kuunga mkono mamlaka ya eneo na umoja wa Somalia.
Mjadala kuhusu tafsiri ya Azimio Na. 2758 unaendelea kuwa sehemu ya mvutano mpana wa kidiplomasia kuhusu hadhi ya Taiwan na nafasi yake katika taasisi za kimataifa.
Wakati China ikisisitiza kuwa azimio hilo linaunga mkono kanuni ya China Moja na kuondoa uwezekano wa uwakilishi wa kimataifa wa Taiwan kama chombo tofauti, Taiwan inaendelea kupinga tafsiri hiyo na kusisitiza kwamba azimio lenyewe halitaji Taiwan kwa jina.
Tags
China
China na Somalia
China na Taiwan
Habari
Kimataifa
Mvutano Somalia na Somaliland
Mvutano Taiwan na China
Somalia
Taiwan
Taiwan na Somaliland
