NA DIRAMAKINI
MKUU wa Wilaya ya Hai, Mheshimiwa Hassan Bomboko amewapongeza watumishi, watendaji wa serikali na wafanyabiashara wa wilaya hiyo kwa kufanya kazi nzuri inayochangia maendeleo na ustawi wa wananchi.
Pongezi hizo amezitoa katika baraza la wafanyabishara wilayani humo ambapo amesisitiza kuwa, hatua hiyo ni muhimu kwa ustawi bora wa wananchi, wilaya na Taifa kwa ujumla.Kuhusu majukumu makuu ya wilaya, Mheshimiwa Bomboko ameeleza kuwa, kazi ya mkuu wa wilaya na kamati yake inajumuisha ulinzi wa raia na mali zao, kusimamia shughuli za maendeleo, pamoja na kusimamia sheria zote zinazoelezwa na wataalamu.
Amebainisha kuwa,kamati ya usalama ya wilaya inasimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazowasilishwa na wataalamu ili kulinda amani na usalama.
Vilevile, amewapongeza watumishi wote wanaotoka serikali kuu hadi serikali za mitaa na taasisi mbalimbali kwa kufanya kazi kubwa na nzuri inayofaa.
Mheshimiwa Bomboko amesema kuwa, hali ya biashara katika wilaya hiyo iko vizuri zaidi huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiendelea kurekodi matokeo changa ya mapato.
Pia,amekumbushia maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ili waweze kufanikiwa na kuleta tabasamu kwa wananchi.
"Wilaya ya Hai inaendelea kuwa kitovu cha amani,usalama na mazingira mazuri ya biashara kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya viongozi,watumishi na wananchi."