NA DIRAMAKINI
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya uteuzi wa Katibu Mkuu mpya pamoja na kufanya mabadiliko katika baadhi ya Kurugenzi zake.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 28,2026 na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya shirikisho hilo.
Mabadiliko hayo yametangazwa leo katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya Rais wake Wallace Karia.
Katika uteuzi huo Evans Mgeusa amekuwa Katibu Mkuu mpya wa TFF akijaza nafasi ya Oscar Mirambo ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo. Kabla ya uteuzi huo, Mgeusa alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NIOREFA).
Oscar Mirambo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu wakati Mustapha Yusuph anakuwa Mkurugenzi mpya wa Fedha.
Katika mabadiliko hayo, Kurugenzi ya Sheria, Habari, na Masoko imegawanywa na kuwa Kurugenzi tatu tofauti.
Walioteuliwa kuongoza Kurugenzi hizo ni Hassan Njama (Biashara na Masoko), Boniface Wambura (Sheria), na Cliford Ndimbo (Habari na Mawasiliano).
Tags
Breaking News
Habari
Kurugenzi za TFF
Michezo
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
TFF Tanzania
Uteuzi
Wallace Karia
