Kuelekea Mvua za El Niño: Mhandisi Sambamba atoa maelekezo kwa wamiliki wa migodi na maafisa wakazi wa mikoa

🔶Aagiza maboresho ya taratibu za migodi, ukaguzi wa maduara, mabwawa ya tope sumu na maandalizi ya dharura

KAHAMA-Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewaelekeza wachimbaji wadogo, wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi nchini kuchukua hatua za haraka kujiandaa na kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba hadi Desemba,mwaka huu ikiwemo kuongeza kasi ya ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji (maduara), mabwawa ya kuhifadhia tope sumu na kuimarisha mipango ya dharura.
Mhandisi Samamba ametoa maelekezo hayo leo Septemba 28, 2026 wilayani Kahama mkoani Shinyanga wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo.

Amesema,tahadhari hiyo inazingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa mvua kubwa kuliko wastani katika kipindi hicho.

Pia, amesema mvua hizo zinaweza kuathiri shughuli za uchimbaji na kusababisha madhara kwa watu, mazingira, miundombinu na uzalishaji iwapo hatua stahiki za tahadhari hazitachukuliwa mapema.

“Wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa kuboresha taratibu za usalama ili ziakisi hali ya mvua kubwa, kuongeza ukaguzi wa maduara na mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, pamoja na kuhakikisha kila mgodi una mpango wa dharura unaoeleweka na kutekelezeka,” amesema.
Amesema,Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa, hivyo maandalizi hayo ni muhimu ili shughuli za uchimbaji ziendelee kwa usalama na tija.

Mhandisi Samamba amesema, miongoni mwa hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa ni kuporomoka kwa maduara na kuta za migodi kutokana na miamba kulainika na kupoteza uimara, mafuriko ndani ya migodi, kudhoofika kwa mihimili inayoshikilia miamba, pamoja na kufurika au kudhoofika kwa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu.

Amesema, pia mazingira yasiyo safi na maji yaliyotuama yanaweza kuongeza hatari za kiafya kwa wachimbaji na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.

Kwa mujibu wa Mhandisi Samamba, wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa kuhakikisha hakuna mchimbaji anayeingia au kuendelea kufanya kazi chini ya ardhi wakati wa mvua kubwa au mara baada ya mvua kukatika iwapo hali ya eneo husika si salama.

Aidha, amewaagiza kuhakikisha maduara yanakaguliwa kila siku kabla ya kazi kuanza na sehemu zote dhaifu kuimarishwa kwa kutumia mihimili imara ya miti au chuma kulingana na mahitaji ya kiusalama.
Amesema,mifereji inayozunguka midomo ya maduara na maeneo ya kazi inapaswa kujengwa na kusafishwa mara kwa mara, huku matuta, kingo, mawe na vifusi vikitumika katika maeneo yanayohitaji ulinzi ili kuzuia maji ya juu ya ardhi kuingia kwenye migodi

“Kila mgodi unapaswa kuwa na pampu za kuvuta maji pamoja na mafuta ya kutosha ili kuwezesha kuchukua hatua za haraka endapo maji yatajaa kwenye mashimo,” amesema.

Kuhusu mabwawa ya kuhifadhia tope sumu (TSF), Mhandisi Samamba amewataka waendeshaji wa migodi kuhakikisha mabwawa hayo yana nafasi na uimara wa kutosha kupokea ongezeko la maji wakati wa mvua, huku ukaguzi wa kingo, mifereji, kiwango cha maji, dalili za kuvuja na mmomonyoko ukifanyika kwa wakati.

Amesema, hatua hizo ni muhimu katika kuzuia madhara kwa binadamu, wanyama, mimea na mazingira.

Mhandisi Samamba pia amesisitiza kuzingatiwa kwa taratibu za usalama wakati wa ulipuaji, akielekeza kuhakikisha watu wote wanatoka katika eneo la tukio na kufika umbali salama kabla ya ulipuaji, na kurejea baada ya muda uliowekwa kwa mujibu wa taratibu za usalama.

Amesema, zamu za wachimbaji zinapaswa kusimamiwa kwa kuzingatia uwezo wa watendaji ili kuzuia uchovu unaoweza kuongeza uwezekano wa kutokea kwa ajali.

Aidha, amewaelekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na Kanuni za Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010, na kuchukua hatua stahiki pale ukiukwaji unapobainika.

Amesema,ukaguzi wa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, maeneo ya kuhifadhi miamba taka na miundombinu mingine ya migodi unapaswa kuongezwa kabla na wakati wa mvua, huku kasoro zinazoweza kuhatarisha usalama zikishughulikiwa mara moja.

Amesisitiza kuwa,kila mgodi unapaswa kuwa na mpango wa dharura unaoeleweka kwa watendaji, unaoainisha namna ya kutoa taarifa, kuokoa watu, kusimamisha shughuli pale inapobidi na kuwasiliana na mamlaka husika.
Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya wachimbaji wa madini kutumia mitandao yao kutoa elimu kwa wanachama na kuwataka wachimbaji kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzitumia katika kupanga shughuli zao za kila siku.

“Kaeni na wachimbaji, wasikilizeni hoja zao na mzitatue kwa kushirikiana. Tusifanye kazi kwa maelekezo pekee, bali kwa ushirikiano,” amesema.

Amesema,usalama haupaswi kuchukuliwa kuwa gharama inayopunguza uzalishaji, kwa kuwa ajali inaweza kusababisha kusimama kwa shughuli za uchimbaji, kuharibu miundombinu, kuathiri mazingira na jamii na kusababisha kupoteza maisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakaguzi wa Migodi Tanzania, Shija Mussa amesema, wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto ya maji kujaa kwenye mashimo wakati wa uchimbaji na kuiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa mitambo mikubwa ya kunyonya maji (heavy-duty pumps) pamoja na vifaa vingine vya dharura.

Amesema,mitambo hiyo inapaswa kuwekwa katika maeneo ya kimkakati ili iweze kutumika kwa haraka wakati wa dharura.

Awali, Mkurugenzi wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema, mafunzo hayo yamelenga kuwapa wachimbaji wadogo elimu na uzoefu kuhusu namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mvua kubwa.

Amesema, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini imeamua kuchukua hatua mapema baada ya kutolewa kwa tahadhari ya mvua, ambapo wataalamu wanawasilisha mada kuhusu usalama wa migodi, mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, maeneo ya kuhifadhi miamba taka, udhibiti wa mafuriko na mipango ya dharura.
Mhandisi Swedi amesema, mafanikio ya mafunzo hayo yataonekana kupitia utekelezaji wa vitendo katika maeneo ya uchimbaji, akiwataka washiriki kurejea katika maeneo yao ya kazi, kufanya tathmini, kubaini maeneo hatarishi na kurekebisha kasoro kabla ya madhara kutokea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here