ZANZIBAR-Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Cleophace Magesa kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi amewaongoza Maafisa, Wakaguzi, Askari wa vyeo mbalimbali pamoja na waombolezaji wengine kuaga mwili wa aliyekuwa askari Polisi Konstable Leodiga Jonas Mbunda aliyefariki tarehe 25 Septemba 2026 kwa ajali ya gari iliyotokea huko Fuoni Nyumba Mbili Wilaya ya Magharibi B" Mkoa wa Mjini Magharibi.
ACP Magesa ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao huku akiwataka askari kuiga mfano mwema wa marehemu Leodiga ambaye enzi za uhai wake wakati akilitumikia Jeshi la Polisi katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mjini Magharibi alikuwa na utendaji bora uliotukuka ikiwemo utii na uadilifu.
Mwili wa marehemu Leodiga Jonas Mbunda, umesafirishwa Septemba 26,2026 kuelekea mkoani Ruvuma kwa ajili ya taratibu nyingine za maziko.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.





