NA DIRAMAKINI
MUFTI na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt.Abubakar Zubeir Bin Ally ametoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa majukumu kwa mwanamke aliyefiwa na mume wake wakati akiwa katika kipindi cha eda, akisema Sheria ya Kiislamu inaruhusu kuendelea na majukumu muhimu yanayohitaji uwepo na uangalizi wake binafsi.
Ufafanuzi huo unalenga kuweka wazi namna ambavyo masharti ya eda yanavyoweza kuhusishwa na mazingira halisi ya maisha, hasa pale mwanamke anapokuwa na majukumu ambayo hayawezi kuhamishiwa kwa mtu mwingine.
Akizungumza Jumatano katika Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) jijini Dar es Salaam, Sheikh Dkt. Zubeir amesema kuwa, mwanamke aliyepo katika eda anaweza kutekeleza majukumu ambayo yanahitaji yeye mwenyewe kuwepo au kuyasimamia, mradi atekeleze wajibu huo kwa kuzingatia masharti na taratibu zilizowekwa na Sheria ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa Mufti huyo, msingi wa suala hilo ni kutambua kwamba baadhi ya majukumu yanaweza kutekelezwa na watu wengine, wakati mengine yanamhitaji moja kwa moja mhusika kutokana na nafasi au wajibu alionao.
Amesema, endapo jukumu fulani ni la lazima na haliwezi kukabidhiwa kwa mtu mwingine, utekelezaji wake haupaswi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ni ukiukaji wa masharti ya eda, iwapo mwanamke husika anaendelea kuzingatia taratibu zinazotakiwa katika kipindi hicho.
Tags
Dkt.Abubakar Zubeir Bin Ally
Eda
Mjane akiwa Eda
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania
Mufti wa Tanzania
Sheria ya Kiislamu