KIGOMA-Septemba 3,2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mheshimiwa Maila M. Makonya (PRM) na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Bw.Balamu Kisumo limefunguliwa shauri la uhujumu uchumi Namba ECO.19924/2026 kati ya Jamhuri dhidi ya Bw.Leonard Alfonsi Mosha (31) ambaye alikuwa muuguzi katika Zahanati ya Bunyambo.
Mshtakiwa anakabiliwa na kosa la ubadhirifu na ufujaji kinyume na kifungu cha 28(1) PCCA Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2023 baada ya kufanya ubadhirifu wa dawa za binadamu zenye thamani ya Shilingi 2,020,345.36.
Mshtakiwa kwa kipindi cha mwezi Novemba,2023 wakati akiwa muuguzi na mtunza dawa Zahanati ya Bunyambo alikuwa anaomba dawa kwenye zahanati mbalimbali ambazo aliziomba kwa matumizi ya Zahanati ya Bunyambo,lakini alikuwa anatumia dawa hizo kwa maslahi yake binafsi.
Baada ya kusomewa shtaka lake, Mshtakiwa alikana shtaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya mahakama.Shauri hilo limepangwa tena Septemba 21,2026 kwa ajili ya uwasilishaji wa hoja za awali (PH).
Tags
Habari
Mahakamani Leo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania
Wizi wa Dawa Zahanati
