NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Msumbiji (SERNIC) imewakamata raia wawili wa Ghana wanaotuhumiwa kujihusisha na utapeli wa mtandao na uhamishaji haramu wa fedha kupitia mifumo ya kibenki.
Watuhumiwa hao wenye umri wa miaka 34 na 40, walikamatwa katika Jiji la Chimoio mkoani Manica katikati mwa Msumbiji, baada ya vyombo vya usalama kuwabaini wakiwa na vifaa na nyaraka kadhaa zinazodaiwa kutumika katika shughuli hizo.
Kwa mujibu wa SERNIC, wakati wa kukamatwa kwao watuhumiwa hao walikutwa na mashine tano za Point of Sale (POS), kadi 49 za benki pamoja na simu nne za mkononi.
Vifaa hivyo vinadaiwa kutumika katika kufanya miamala na uhamishaji wa fedha kwa njia zisizo halali, huku mamlaka zikianza uchunguzi kubaini chanzo cha kadi hizo, matumizi ya vifaa hivyo na mtandao mpana ambao huenda ulihusika katika operesheni hiyo.
Msemaji wa SERNIC katika mkoa wa Manica, Paulo Candieiro amewaambia waandishi wa habari kuwa,kadi za benki zilizokamatwa si za taasisi za fedha za ndani ya Msumbiji, jambo ambalo limeongeza mashaka kuwa watuhumiwa walikuwa wakihamisha fedha kwenda nje ya nchi ikiwemo nchini kwao Ghana.
“Vifaa vya POS na kadi hizo si vya hapa nchini. Tunaamini walikuwa wakitumia vifaa hivyo katika kufanya udanganyifu wa kibenki. Uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chimbuko la kadi na vifaa hivyo, pamoja na kuwabaini watu wengine ambao huenda wanahusika na kundi hilo,”amesema Candieiro.
Amesema,mamlaka zinaendelea kuchunguza namna miamala hiyo ilivyokuwa ikifanyika, pamoja na kubaini iwapo kulikuwa na watu wengine waliokuwa wakishirikiana na watuhumiwa hao.
“Bado tunaendelea na kazi ya kuelewa namna miamala hiyo ilivyotekelezwa na kama kuna watu wengine waliohusika. Mtu yeyote atakayebainika kuhusishwa na mpango huu atafikishwa mbele ya sheria,”ameongeza.
Aidha, kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunafanyika wakati ambapo matumizi ya mifumo ya kidijitali katika huduma za kifedha yakiendelea kuongezeka katika nchi nyingi za Afrika, hali inayosababisha pia changamoto mpya kwa mamlaka za usalama katika kukabiliana na uhalifu unaotumia teknolojia.
SERNIC inaendelea na uchunguzi ili kubaini mtandao mzima wa operesheni hiyo, thamani ya fedha zinazodaiwa kuhamishwa, pamoja na uwezekano wa kuwepo kwa washirika wengine ndani au nje ya Msumbiji.(NA)
Tags
Ghana
Ghana na Msumbiji
Habari
Kataa Utapeli
Kimataifa
Mamlaka ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Msumbiji (SERNIC)
Msumbiji
Raia wa Ghana
Uhamishaji Haramu wa Fedha
Utapeli Mtandaoni
