ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa madrasa katika kujenga kizazi chenye elimu ya dini, maadili mema na misingi imara ya malezi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Septemba 18, 2026 katika Dua Maalum ya kuliombea Taifa, viongozi wa nchi na kuomba kwa Mwenyezi Mungu kuiepusha Zanzibar na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa pamoja na El Niño, iliyofanyika Almadrasat Swifat Nabawiyatil Karimah, Msolopa Kilimani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema ushirikiano kati ya walimu wa madrasa, wazazi, walezi, viongozi wa dini na jamii ni muhimu katika malezi ya watoto na vijana, hususan katika kipindi hiki cha matumizi makubwa ya teknolojia na mitandao ya kijamii.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na amani, pamoja na kuchukua tahadhari na kuzingatia taarifa na maelekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) na Serikali kuhusu mvua kubwa zinazotarajiwa.











