DAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Waislamu na wananchi kwa ujumla kuendeleza umoja, upendo, mshikamano na kuheshimiana katika jamii, akisisitiza kuwa kujenga jamii yenye amani na maadili mema ni wajibu wa kila mmoja.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Septemba 13,2026 wakati akihutubia Usiku wa Shukrani katika Msikiti wa Istiqaama, uliopo Ilala, Jijini Dar es Salaam, ambapo ameungana na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa dini, waumini na wageni mbalimbali.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa shukrani ni sehemu ya imani na miongoni mwa maadili muhimu yanayopaswa kuendelezwa katika jamii, huku akiwataka Waislamu kuendelea kufanya mema na kushirikiana katika kujenga jamii yenye upendo, amani na mshikamano.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa salamu za pole kwa familia, ndugu, marafiki na waumini wa marehemu Sheikh Ahmed Albadry, aliyewahi kuwa Imam Mkuu wa Msikiti wa Istiqaama na Sheikh Mkuu wa kwanza wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania.
Amesema marehemu Sheikh Ahmed Albadry alitoa mchango mkubwa katika kujenga na kuimarisha umoja wa Waislamu, akieleza kuwa urithi wake katika elimu, uongozi, ibada na kuwaunganisha Waislamu utaendelea kukumbukwa na jamii.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kwa miaka 17, Msikiti wa Istiqaama umekuwa zaidi ya mahali pa ibada, bali umekuwa kituo muhimu cha elimu ya dini, malezi ya vijana, kuimarisha familia, kukuza maadili mema na kuwaunganisha Waislamu.
Ametoa wito kwa viongozi wa dini na waumini kuendeleza moyo wa kujitolea katika kujenga jamii na kuimarisha nyumba za ibada, akisisitiza kuwa kila anayetoa mali, muda, elimu, nguvu au dua kwa ajili ya kujenga jamii anastahili kuthaminiwa.
Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru Wadhamini wa Istiqaama, viongozi wa Msikiti na Jumuiya ya Istiqaama, viongozi wa dini na Serikali pamoja na waumini wote kwa kufanikisha tukio hilo, na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika juhudi za kuimarisha dini, umoja, mshikamano, maadili na maendeleo ya jamii.

















