NA DIRAMAKINI
MHESHIMIWA Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewataka viongozi wa Mikoa na Wilaya nchini kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kudhibiti matumizi na kuelekeza rasilimali zilizopo katika shughuli zilizopangwa na vipaumbele vya maendeleo.
Rais Dkt. Samia ametota maagizo hayo leo Septemba 2, 2026 katika hafla ya uapisho wa Wakuu wa Mikoa na Katibu Tawala wa Mkoa, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar.
Amesema, Mikoa na Halmashauri zote nchini zinapaswa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutumia sehemu ya mapato hayo kugharamia shughuli za maendeleo, ili kupunguza utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu.
"Kila mwenye eneo lake la utawala ajitahidi kuhakikisha mambo yanaenda katika eneo lake; si kila kitu kitoke kwenye Hazina ya Serikali,"amesema Rais Dkt.Samia.
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2025 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji kila kiongozi kusimamia matokeo katika eneo lake, akizingatia ukubwa wa malengo, muda uliopo na uhalisia wa rasilimali.
Katika kutekeleza wajibu huo, amezitaka Halmashauri zote nchini kubaini mapato ambayo hayakusanywi ipasavyo na kuelekeza fedha zinazopatikana katika utekelezaji wa miradi, hususan ile ya kipaumbele, ikiwemo afya na elimu.
Akizungumzia uwezeshaji wa wananchi, Rais Dkt. Samia amezipongeza baadhi ya Halmashauri nchini zilizofanya vizuri katika utoaji wa usimamizi wa mikopo ya asilimia 10, huku akizitaka Halmashauri zinazosuasua kuimarisha utekelezaji wake.
Vilevile, ameagiza mikopo hiyo ielekezwe kwa vikundi vyenye miradi inayozalisha, na kumbukumbu sahihi ziwekwe kuonesha wanufaika, miradi iliyofadhiliwa na marejesho yaliyofanyika.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuimarisha usimamizi wa wafanyabiashara wadogo, akisema kulegalega kwa usimamizi katika eneo hilo kumewafanya wengi wao kurejesha shughuli zao za biashara katika maeneo yasiyo rasmi.
Amezielekeza Halmashauri kutumia mapato ya ndani kupanua na kujenga masoko mapya, pamoja na kupanga njia mpya za usafiri kuyafikia maeneo hayo, ili yawe na shughuli endelevu za kibiashara na kuwavutia wafanyabiashara kuhamia katika maeneo rasmi.
Sambamba na hilo, Rais Dkt. Samia amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia upangaji na matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro baina ya wakulima, wafugaji, wananchi na maeneo ya hifadhi.
Katika sekta ya elimu, ameagiza Mikoa kuanza mapema maandalizi ya kuwapokea wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2028, ili mahitaji yote muhimu yatambuliwe na kushughulikiwa kwa wakati.
Amesema, idadi ya wanafunzi itaongezeka kwa sababu wahitimu wa Darasa la Sita na Darasa la Saba watajiunga na Kidato cha Kwanza kwa wakati mmoja, kutokana na mabadiliko ya sera ya elimu.
Akirejea utabiri wa mvua za El Niño, Rais Dkt. Samia amewataka viongozi wa Mikoa na Halmashauri kufanya maandalizi ya mapema, sambamba na kuimarisha usimamizi wa mazingira na usafi mijini.
Kuhusu usafi mijini, ameagiza kandarasi kutolewa kwa kampuni zenye vifaa na uwezo wa kutekeleza kazi hiyo kwa ufanisi, badala ya kuwapatia wakandarasi wasiokidhi sifa, uwezo na mahitaji.
Walioapishwa kuwa Wakuu wa Mikoa ni Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (Mbeya), Mhe. Alexander Pastory Mnyeti (Geita), Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo (Pwani) na Mhe. CP Salum Rashid Hamduni (Mwanza).
Wakuu wa Mikoa waliohamishwa ni Mhe. Martine Reuben Shigela kwenda Manyara, Mhe. Said Mohamed Mtanda kwenda Simiyu, Mhe. Abubakar Mussa Kunenge kwenda Songwe, Mhe. Beno Moris Malisa kwenda Tabora, Mhe. Adam Kighoma Malima kwenda Lindi na Mhe. Queen Cuthbert Sendiga kwenda Morogoro.
Aliyeapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ni Bw. Richard Marcellino Kayombo. Makatibu Tawala waliohamishwa ni Bw. Balandya Mayuganya Elikana kwenda Mbeya, Dkt. Fatuma Ramadhan Mganga kwenda Mwanza, Bi. Pili Hassan Mnyema kwenda Shinyanga, na Bw. Rodrick Lazaro Mpogolo kwenda Singida.
Tags
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Halmashauri za Tanzania
Maagizo ya Rais Samia
Uapisho wa Viongozi Mbalimbali Ikulu



