Rais Dkt.Samia atoa maagizo mazito kwa wakuu wa mikoa

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi walioteuliwa na kuapishwa hususan Wakuu wa Mikoa, kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na kutambua kuwa dhamana waliyopewa ni wajibu wa kusimamia shughuli zote za Serikali katika maeneo yao.
Ametoa agizo hilo leo Septemba 2, 2026 katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar muda mfupi baada ya kuwaapisha viongozi hao, akisisitiza kuwa uteuzi wao ni ishara ya imani kubwa waliyopewa na Serikali.

Walioapishwa kuwa Wakuu wa Mikoa ni Mhe. Jumanne Abdallah Sagini (Mbeya), Mhe. Alexander Pastory Mnyeti (Geita), Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo (Pwani) na Mhe. CP Salum Rashid Hamduni (Mwanza).

Wakuu wa Mikoa waliohamishwa ni Mhe. Martine Reuben Shigela kwenda Manyara, Mhe. Said Mohamed Mtanda kwenda Simiyu, Mhe. Abubakar Mussa Kunenge kwenda Songwe, Mhe. Beno Moris Malisa kwenda Tabora, Mhe. Adam Kighoma Malima kwenda Lindi na Mhe. Queen Cuthbert Sendiga kwenda Morogoro.

Aliyeapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ni Bw. Richard Marcellino Kayombo. Makatibu Tawala waliohamishwa ni Bw. Balandya Mayuganya Elikana kwenda Mbeya, Dkt. Fatuma Ramadhan Mganga kwenda Mwanza, Bi. Pili Hassan Mnyema kwenda Shinyanga, na Bw. Rodrick Lazaro Mpogolo kwenda Singida.

Rais Dkt.Samia amesema,viongozi hao wanapaswa kutumia dhamana hiyo kuhakikisha kero na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati, badala ya kusubiri kila jambo lifikishwe ngazi ya juu ya Serikali.

Pia amesema, kikatiba madaraka ya Rais yamekasimiwa kwa viongozi wa Serikali katika maeneo mbalimbali, hivyo Wakuu wa Mikoa wanapaswa kutambua uzito wa nafasi zao na kuchukua hatua katika kushughulikia masuala yanayowahusu wananchi.

Amesema,mtazamo huo unapaswa kumsaidia Mkuu wa Mkoa kutekeleza majukumu yake kwa ujasiri, uwajibikaji na kujenga utamaduni wa kutatua matatizo ya wananchi badala ya kuyapitisha kutoka ofisi moja kwenda nyingine.

Hata hivyo, Rais Samia amewatahadharisha viongozi hao dhidi ya kutumia madaraka waliyopewa kujiona kuwa watawala au wafalme wa maeneo wanayoyaongoza, akisisitiza kuwa dhamana ya uongozi ni ya kuwatumikia wananchi.
"Hatujawapeleka kuwa wafalme wa maeneo hayo, bali kuwa watumishi wa kutumikia watu,”amesema.

Amesema,Mkuu wa Mkoa anapaswa kuutazama mkoa anaouongoza na wananchi wake kama sehemu ya wajibu wake wa moja kwa moja, huku akichukulia changamoto zinazowakabili wananchi kuwa ni changamoto zinazomhusu yeye binafsi kama kiongozi.

“Nendeni mkachape miguu kwelikweli katika kuwatumikia wananchi, matatizo ya mkoa ni ya kwenu,” amesisitiza.

Rais amewataka viongozi hao kuongoza kwa uzalendo, uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia maslahi mapana ya wananchi, akisisitiza kuwa dhamana ya uongozi inapaswa kuonekana kupitia matokeo ya kazi wanazozifanya katika maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewaagiza viongozi wa Serikali za Mikoa na Halmashauri kutafuta namna bora ya kusimamia wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara mitaani, badala ya kutumia nguvu, kuwanyang’anya bidhaa zao au kuwafanyia vitendo vya ukatili.

Amesema,licha ya Serikali kujenga masoko makubwa kwa ajili ya wafanyabiashara, baadhi ya wafanyabiashara wadogo wameanza kurejea mitaani kwa kasi, jambo linalohitaji viongozi kutafuta suluhisho la kudumu badala ya kukabiliana nao kwa nguvu.
"Twende tukawasimamie si kwa kuwapiga fimbo kwa kutumia mgambo, kwa kuwanyang’anya vitu vyao na kuwapiga mateke, hapana, bali kwa mipango mizuri itakayowafanya warudi kwenye masoko,” amesema.

Rais Samia amesema changamoto ya wafanyabiashara wadogo kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi inapaswa kushughulikiwa kwa mipango inayozingatia hali halisi ya wafanyabiashara hao na mahitaji ya wananchi.

Amesema,Serikali za Mikoa na Halmashauri zinapaswa kuwa wabunifu katika kupanga maeneo ya biashara ili wafanyabiashara wadogo wapate mazingira salama na rasmi ya kuendesha shughuli zao bila kuvuruga shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

Rais Samia pia amezitaka halmashauri kuongeza juhudi katika ujenzi wa masoko kwa kutumia rasilimali na fursa zinazopatikana katika maeneo yao, akisisitiza kuwa Serikali za Mitaa haziwezi kusubiri kila mradi utekelezwe na Serikali Kuu.
"Halmashauri jitahidini mjenge masoko mengine, si kila soko kwenye Halmashauri zenu litajengwa na Serikali, nyinyi pia ni Serikali,” amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here