Rwanda yaandaa Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Mawaziri na Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa ESAAMLG

KIGALI-Rwanda imekuwa nchi Mwenyeji wa Mikutano ya Mwaka ya Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kupambana na Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi (ESAAMLG), inayofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Kigali, kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 5, 2026.
Mikutano hiyo inajumuisha Mkutano wa 52 wa Maafisa Waandamizi na Mkutano wa 26 wa Baraza la Mawaziri, pamoja na Mkutano wa 9 wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

Mikutano hii huwakutanisha viongozi wa Serikali katika ngazi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Fedha, Katiba na Sheria, Mambo ya Ndani na maafisa waandamizi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo kwa upande wa Tanzania utawashirikisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Homera na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dkt. Seif Abdallah Shekalage.

Wengine ni Mkurugenzi wa Mashtaka DPP Sylvester Mwakitalu, pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, Kamishna wa Kitengo cha FIU, Bw. Majaba Magana na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bi. Sauda Msemo, wakuu wa taasisi, wataalamu wa sekta ya fedha, wasimamizi wa taasisi za kifedha na wadau wengine wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali za ukanda huo.

Lengo la mkutano huo ni kuimarisha juhudi za pamoja za kupambana na utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi, na ufadhili wa kuenea kwa silaha za maangamizi, huku nchi wanachama zikihimizwa kujenga mifumo yenye matokeo ya moja kwa moja badala ya kuishia katika utekelezaji wa masharti ya kiufundi pekee.
Kauli mbiu ya mikutano ya mwaka huu inalenga kuweka msukumo wa kutoka kwenye kufuata matakwa ya kiufundi kwenda kwenye kuonyesha matokeo halisi katika mifumo ya kupambana na uhalifu wa kifedha ndani ya ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi, maandalizi hayo yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Sekretariati ya ESAAMLG, Serikali ya Rwanda, Wizara ya Fedha na Mipango ya Uchumi ya Rwanda, pamoja na Kituo cha Ujasusi wa Fedha cha Rwanda.

Ushirikiano huo unaelezwa kuwa sehemu ya dhamira ya Rwanda ya kuendelea kuimarisha usimamizi wa mifumo ya fedha na kuongeza mchango wake katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kifedha barani Afrika.

Wachambuzi wa masuala ya fedha wanaeleza kuwa,mkutano huo ni muhimu kwa sababu unatoa nafasi kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zilizopo, na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha uwazi, usalama wa sekta ya fedha na ushirikiano wa kikanda.
Ushiriki wa Tanzania katika ESAAMLG una umuhimu mkubwa kwa sababu unaiwezesha nchi kuendelea kuwa sehemu ya juhudi za kikanda za kupambana na utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na uhalifu mwingine wa kifedha unaoweza kudhoofisha uchumi wa taifa.

Aidha,katika mikutano hii, Serikali ya Tanzania hupata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za usimamizi wa mifumo ya kifedha na kuimarisha uwezo wa taasisi zake katika kusimamia uwazi, uadilifu na usalama wa sekta ya fedha.

Kwa upande mwingine, kushiriki mkutano huo kunatoa nafasi kwa Tanzania kutetea maslahi yake ya kiuchumi na kuonyesha dhamira yake ya kuzingatia viwango vya kikanda na kimataifa katika usimamizi wa fedha.

Ushiriki huo pia huongeza ushirikiano kati ya Tanzania na nchi nyingine wanachama katika masuala ya uchunguzi wa miamala shuku, ufuatiliaji wa fedha haramu na ujenzi wa mazingira salama ya biashara na uwekezaji, jambo ambalo ni muhimu kwa kukuza imani ya wawekezaji na kuimarisha maendeleo ya uchumi.
Kwa Rwanda, kuwa mwenyeji wa mkutano huo kunatazamwa kama ishara ya kuongezeka kwa nafasi yake katika mijadala ya kikanda kuhusu uadilifu wa mifumo ya kifedha, uthibiti wa hatari za kifedha na ushirikiano wa kimataifa dhidi ya uhalifu wa kifedha.

Mkutano huo unatarajiwa kutoa maazimio na mapendekezo yatakayosaidia nchi wanachama kuimarisha sera, sheria na mifumo ya taasisi zao kwa lengo la kulinda uchumi wa mataifa yao dhidi ya matumizi haramu ya mifumo ya kifedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here