TANGA-Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Gemini Mushy, Mkuu wa Kitengo cha INTERPOL, Ofisi ya DCI Dodoma, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura tarehe 05 Septemba, 2026 ameongoza Maofisa,Wakaguzi, Askari wa vyeo mbalimbali na Watumishi raia kuaga mwili wa aliyekuwa Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP) Yusuf Kijali Ilembo katika Makaburi ya Vibaoni, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga.
DCP Gemini Mushy ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na Askari kwa kuondokewa na mpendwa wao na kuwaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi, sambamba na kuyaishi mambo yote mema yaliyofanywa na marehemu kipindi cha uhai wake.
Pia, kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi, ametoa shukrani kwa viongozi wa Jeshi la Polisi, Maofisa, Wakaguzi, Askari wa vyeo mbalimbali, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote walioshiriki katika msiba na maziko ya marehemu.
ACP Mchunguzi ametoa shukrani za pekee kwa DCP Gemini Mushy kwa kuwaongoza Maofisa, Wakaguzi, Askari wa vyeo mbalimbali na waombolezaji katika kutoa heshima za mwisho kwa marehemu.
Marehemu SACP Yusuf Kijali Ilembo amezikwa katika Makaburi ya Vibaoni, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga, huku familia, ndugu, jamaa na waombolezaji wakimuombea Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.














