NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimekubaliana kuondoa suala la mafuta na gesi asilia katika Orodha ya Mambo ya Muungano, hatua inayolenga kuweka wazi zaidi mgawanyo wa majukumu ya usimamizi wa sekta hiyo kati ya pande mbili za Muungano.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe, Mhe. Rashid Habib Ali Rashid, bungeni jijini Dodoma, Septemba 1, 2026.
Mbunge huyo aliitaka Serikali kueleza mpango iliyonao wa kuliondoa suala la mafuta na gesi katika Orodha ya Mambo ya Muungano, akitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza azma hiyo.
Akijibu, Mhe. Kwagilwa alisema,Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar tayari zimekubaliana kuondoa jambo la 15 linalohusu maliasili ya mafuta, ikiwemo mafuta yasiyochujwa ya motokaa, mafuta ya aina ya petroli na aina nyingine za mafuta au bidhaa zake, pamoja na gesi asilia katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Alisema, hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba kwa sasa suala la mafuta na gesi asilia tayari linasimamiwa na kila upande kupitia mifumo yake ya kisheria na kitaasisi.
Kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema, imeweka mfumo wa kisheria kupitia Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015, ambayo chini ya Kifungu cha 11 imeanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).
PURA ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli zinazohusiana na mkondo wa juu wa sekta ya petroli, hususan utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo imeweka mfumo wake wa kisheria na kitaasisi kupitia Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Na. 6 ya mwaka 2016.
Sheria hiyo imeanzisha Mamlaka ya Udhibiti, Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) pamoja na Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC), taasisi zinazoshughulikia masuala ya sekta hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, Mhe. Kwagilwa alisema,hatua ya Zanzibar kutunga sheria na kuanzisha taasisi zake za kusimamia sekta ya mafuta na gesi inaonesha kuwa suala hilo tayari linashughulikiwa kwa utaratibu wa kila upande.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na Mheshimiwa Mbunge ambaye amesema kwamba Baraza la Wawakilishi lilisharidhia na lilishawasilisha kutaka suala hili liondolewe na ndiyo maana Baraza la Wawakilishi limetunga sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa suala hilo tayari linashughulikiwa na kila upande kwa kutumia sheria na taasisi zake, hakuna mgongano unaoweza kuzuia hatua ya kuliondoa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
“...hivyo linashughulikiwa katika kila upande, hivyo halina hoja kinzani,” alifafanua Naibu Waziri.
Kauli hiyo inakuja wakati ambapo suala la mgawanyo wa mamlaka na majukumu katika usimamizi wa rasilimali za mafuta na gesi limeendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji ufafanuzi ndani ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa maelezo ya Serikali, kuondolewa kwa suala hilo katika Orodha ya Mambo ya Muungano kutatoa nafasi kwa kila upande kuendelea kusimamia sekta ya mafuta na gesi asilia kwa mujibu wa sheria, taasisi na mifumo yake ya kiutawala.
Hatua hiyo pia inaashiria mwendelezo wa jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kushughulikia masuala yanayohusu mgawanyo wa mamlaka na majukumu kati ya pande mbili za Muungano.
Hata hivyo, utekelezaji wa makubaliano hayo unahitaji kufuata taratibu za kikatiba na kisheria zinazohusika katika mabadiliko ya Orodha ya Mambo ya Muungano.
Vilevile, Serikali imesisitiza kuwa suala la mafuta na gesi asilia tayari lina mifumo ya usimamizi katika pande zote mbili, huku hatua ya kuliondoa rasmi kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano ikiwa sehemu ya mchakato unaoendelea wa utekelezaji wa makubaliano kati ya SJMT na SMZ.
