Serikali yajivunia mchango wa TBA katika kustawisha Sekta ya Fedha

ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali inajivunia mchango wa sekta ya kibenki katika kustawisha sekta ya fedha, ambayo ni nguzo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Mhe. Hemed ameyasema hayo alipohutubia katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), iliyofanyika tarehe 4 Septemba 2026, Unguja, Zanzibar.

“Leo tunapoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TBA, tunajivunia sekta ya kibenki ambayo imekuwa muhimu katika ustawi wa sekta ya fedha na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla,” alisema.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho, Tanzania imepitia mageuzi makubwa katika sekta ya kibenki, ambapo huduma za kibenki zimeondokana na utegemezi wa matawi na huduma za ana kwa ana na kuelekea kwenye mifumo ya kidijitali inayounganisha benki, simu za mkononi na mifumo mbalimbali ya malipo, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa wananchi.
"Hatua hiyo imechangia kuleta matokeo chanya, ambapo mamilioni ya Watanzania wameweza kupata huduma za kifedha, mitaji ya biashara, fursa za kuwekeza na kuweka akiba, pamoja na kuchochea uundaji wa ajira na shughuli za uzalishaji, hivyo kuchangia katika kustawisha uchumi wetu,” alisisitiza Mhe. Hemed.

Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Rahma Mahfoudh, alisema kupitia mabenki ambayo ni wanachama wake, Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) umechangia katika kuelekeza rasilimali za fedha kwenye shughuli za uzalishaji, biashara, kilimo, viwanda, makazi, miundombinu na miradi ya kimkakati ya Taifa.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwezi Julai 2026, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 28.1 kwa mwaka ulioishia Juni 2026. Ukuaji huo umeendelea kusaidia shughuli za uzalishaji na uwekezaji, na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na uundaji wa ajira nchini.

Aliongeza kuwa sekta ya fedha inatarajiwa kuwa mhimili muhimu katika kuchochea uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa uchumi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Dira hiyo inalenga kuijenga Tanzania yenye uchumi wa takribani Dola za Marekani trilioni moja. Katika mazingira haya, sekta ya fedha haitakuwa mtazamaji, bali mshirika muhimu katika utekelezaji wa Dira hiyo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania, Bw. Theobald Sabi, alisema hadi mwisho wa mwaka 2025, jumla ya rasilimali za sekta ya benki zilifikia takribani shilingi trilioni 79.4, na kuongezeka hadi takribani shilingi trilioni 84.6 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026. Katika kipindi hicho, mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kukua kwa takribani asilimia 23.
"Haya ni mafanikio yanayoonesha sekta iliyo imara, inayokua na yenye uwezo mkubwa zaidi wa kuchangia maendeleo ya Taifa letu,” alisema.

Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ulianzishwa mwaka 1995 wakati Tanzania ikitekeleza mageuzi makubwa ya sekta ya fedha yaliyolenga kuongeza ushindani, kuhamasisha uwekezaji binafsi, kukuza ubunifu na kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here