TPTU yasukuma hoja 27 za walimu wa shule binafsi Tanzania,yataka Serikali itoe mrejesho

NA DIRAMAKINI

CHAMA cha Walimu na Wafanyakazi wa Shule Zisizo za Serikali Tanzania (TPTU) kimeitaka Serikali kutoa mrejesho rasmi na kuchukua hatua kuhusu hoja 27 za changamoto zinazowakabili walimu, wafanyakazi na wamiliki wa shule zisizo za serikali, ambazo chama hicho kimekuwa kikizifuatilia tangu mwaka 2023.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa TPTU, Mwalimu Julius Mabula Nkoba katika makao makuu ya chama hicho jijini Mwanza.

TPTU imesema hoja hizo, ambazo zinagusa maeneo ya ajira, mazingira ya uwekezaji, kodi na tozo, hifadhi ya jamii, maendeleo ya walimu, usimamizi wa elimu, sera na mifumo ya kiutawala, tayari zimewasilishwa katika ngazi mbalimbali za Serikali na Bunge, lakini baadhi yake bado hazijapatiwa majibu ya mwisho.

Kwa mujibu wa chama hicho, katika hatua ya sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano imekithibitishia kuwa imepokea hoja hizo na kwamba zinafanyiwa kazi kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

TPTU imesema,inathamini hatua hiyo, lakini imeitaka Serikali kuhakikisha mchakato huo unaambatana na ratiba ya utekelezaji, mgawanyo wa majukumu kwa taasisi husika na mrejesho rasmi kwa kila hoja.

“Hatusemi kwamba Serikali haijawahi kupokea changamoto hizi. Serikali ilishazipokea na zimepitia katika hatua mbalimbali. Tunachosisitiza ni kwamba baada ya taasisi ya wananchi kuwasilisha hoja rasmi, ni muhimu kupata mrejesho rasmi,” chama hicho kimesema katika taarifa yake iliyotolewa Agosti 31,2026.

Mchakato ulianza mwaka 2021

TPTU imesema, jitihada za kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo hazikuanza mwaka 2023, bali zilianza mwaka 2021 baada ya chama hicho kupata kibali cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia cha Novemba 29, 2021, chenye Kumbukumbu Na. CA.34/237/01/3.

Kwa mujibu wa chama hicho, kwa kibali hicho kilizunguka mikoa 16 ya Tanzania Bara na kukutana na walimu, wafanyakazi, mameneja na wamiliki wa shule zisizo za serikali ili kusikiliza changamoto zinazowakabili.

TPTU inasema, majadiliano hayo yalibainisha kuwa baadhi ya changamoto hazingeweza kutatuliwa na mwalimu, shule au mwajiri mmoja mmoja, bali zilihitaji hatua za Serikali Kuu kupitia sera, sheria, kanuni na mifumo ya kiutawala.

Mwaka 2022, chama hicho kiliandika kwa vyama vya wamiliki wa shule zisizo za serikali, kikitaka kuwe na ushirikiano wa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.

Barua hiyo ya Agosti 31,2022 yenye Kumbukumbu Na. TPTU/KM/TAMONGSCO/01/22 kwa mujibu wa TPTU, haikujibiwa licha ya chama hicho kusubiri kwa takribani miezi minne.

Barua kwa Rais

Baada ya hapo, TPTU ilimwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Desemba 22,2022 kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. TPTU/IKULU/RAIS/02/22, ikiomba fursa ya kuwasilisha changamoto hizo na kujadili namna ya kuzipatia ufumbuzi.

Chama hicho kinasema baada ya barua hiyo kufika Ikulu, kilielekezwa kuwasilisha hoja hizo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuendelea kuzifuatilia kupitia wizara hiyo kabla ya kurejea Ikulu endapo hakutakuwa na majibu.

Kwa kutekeleza maelekezo hayo, TPTU ilimwandikia Waziri wa Elimu Januari 2, 2023, kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. TPTU/W/WEST/01/23.

Baada ya kukosa majibu kwa mwezi mmoja, chama hicho kilisema kilimkumbusha Waziri huyo na baadaye kufanya hivyo tena.

Hatimaye, kwa barua ya Juni 5, 2023, yenye Kumbukumbu Na. CA.315/372/01/23, TPTU iliitwa Dodoma kwa majadiliano yaliyofanyika Juni 7, 2023.

Katika kikao hicho, chama hicho kiliwasilisha rasmi hoja 27 na, kwa mujibu wa taarifa yake, Waziri alizipokea na kueleza kuwa zingefanyiwa kazi.

Hoja ya mkutano wa wamiliki wa shule

Katika kikao hicho, TPTU pia ilishauri Serikali kuitisha mkutano wa wamiliki wa shule zisizo za serikali ili kusikiliza changamoto zao moja kwa moja.

TPTU inasema ushauri huo ulifanyiwa kazi na mkutano huo ukafanyika Oktoba 10, 2023 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, ukiwashirikisha takribani wamiliki 3,200 wa shule.

Hata hivyo, chama hicho kinasema, licha ya kutoa ushauri wa kufanyika kwa mkutano huo, hakikushirikishwa wala kualikwa.

Kwa mujibu wa TPTU, katika mkutano huo Waziri alieleza kuwa changamoto zilizowasilishwa zingefanyiwa kazi na kwamba Machi 2024 kungekuwa na mkutano mwingine wa kutoa mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa. TPTU inasema mkutano huo wa mrejesho haukufanyika.

Hoja 27 zagawanywa katika makundi manne

TPTU imezipanga hoja zake katika makundi manne makuu ikiwemo mazingira ya uwekezaji na uendeshaji wa shule zisizo za serikali; changamoto za walimu na wafanyakazi; ushirikishwaji wa TPTU katika masuala ya sera na usimamizi wa elimu; pamoja na mifumo ya elimu, utawala na sera.

Mazingira ya uwekezaji

Katika kundi la kwanza, TPTU inataka Serikali itazame upya mazingira ya uwekezaji katika sekta ya elimu, ikisema shule zisizo za serikali zina mchango katika kupanua fursa za elimu, kupunguza mzigo wa Serikali na kutoa ajira.

Chama hicho pia kinataka wawekezaji na waendeshaji wa shule washirikishwe kabla ya kufanyika kwa maamuzi ya kisera yanayohusu sekta hiyo.

Hoja nyingine katika kundi hili ni mapitio ya mfumo wa leseni za biashara na matumizi ya mashine za EFD katika shule, mzigo wa kodi, tozo, ada na michango mbalimbali.

TPTU pia imeomba Serikali kuwa na mpango wa kitaifa wa kukabiliana na majanga makubwa kama COVID-19, ukiwalinda wafanyakazi na wawekezaji katika sekta binafsi.

Chama hicho kinataka pia walimu wa shule zisizo za serikali washirikishwe kikamilifu katika programu za maendeleo ya kitaaluma, ikiwemo mafunzo, warsha na semina.

Aidha, kinataka kuwe na utaratibu bora wa upatikanaji wa vitabu vya kiada na miongozo ya walimu, pamoja na mapitio ya ada za mitihani ya kitaifa na ada za ukaguzi wa shule.

Hoja ya mwisho katika kundi hili inahusu michango ya kijamii inayotozwa kwa lazima, ambapo TPTU inataka kuwe na mwongozo unaotofautisha michango ya hiari na tozo au malipo yanayolazimishwa kisheria.

Haki za walimu na wafanyakazi

Katika kundi la pili, TPTU imeelekeza hoja zake katika ajira, mazingira ya kazi na ustawi wa walimu na wafanyakazi wa shule zisizo za serikali.

Chama hicho kinataka walimu wenye sifa kutoka shule hizo washirikishwe katika usimamizi, usahihishaji na shughuli nyingine zinazohusiana na mitihani ya kitaifa.

TPTU pia imependekeza kuwe na mfumo wa uteuzi na uthibitishaji wa wakuu wa shule, huku wamiliki wakiendelea kuwa na nafasi ya kuteua viongozi hao kwa kuzingatia sifa na uwezo.

Kwa upande wa ajira, chama hicho kimeibua changamoto zinazohusisha usalama wa ajira, mishahara, mazingira ya kazi, mzigo wa kazi, manyanyaso na ucheleweshaji wa mishahara.

TPTU pia imetaka kuimarishwa kwa utekelezaji wa sheria kuhusu utoaji wa mikataba ya ajira, huku ikisisitiza kuwa walimu na wafanyakazi wanapaswa kupewa nyaraka zinazoeleza wazi masharti ya ajira.

Hoja nyingine ni kuhakikisha kima cha chini cha mshahara kinazingatiwa, pamoja na kuweka utaratibu wa kuwawezesha walimu na wafanyakazi wa shule zisizo za serikali kupata bima ya afya.

Chama hicho pia kimeibua changamoto ya wafanyakazi hao kushindwa kukopesheka katika baadhi ya taasisi za fedha na kueleza kuwa kimeanzisha SACCOS kwa wanachama wake kama sehemu ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Katika eneo la hifadhi ya jamii, TPTU imetaka changamoto zinazohusu usajili wa wafanyakazi, uwasilishaji wa michango na usahihi wa taarifa za michango katika mifuko ya hifadhi ya jamii zishughulikiwe.

TPTU yataka kutambuliwa katika sera za elimu

Katika kundi la tatu, TPTU inataka itambuliwe na kushirikishwa kama mdau wa kitaifa anayewakilisha walimu na wafanyakazi wa shule zisizo za serikali.

Chama hicho pia kimeeleza msimamo wake kuhusu Bodi ya Kitaaluma ya Walimu Tanzania, kikisema kinatambua umuhimu wa kuwepo kwa chombo cha kitaaluma kinachowasimamia walimu wote, wakiwemo wanaofanya kazi katika shule zisizo za serikali.

Hata hivyo, TPTU inataka kuhakikisha mfumo huo unakuwa wa haki, wa kitaaluma na unaolinda maslahi ya walimu.

Aidha, chama hicho kinataka walimu na wafanyakazi wa shule zisizo za serikali washirikishwe katika mafunzo, semina, warsha, mijadala na shughuli nyingine za kitaaluma kulingana na sifa na taaluma zao.

Mapendekezo kuhusu mfumo wa elimu

Katika kundi la nne, TPTU imewasilisha mapendekezo yanayohusu uhamaji wa wanafunzi kutoka shule moja kwenda nyingine, ikitaka mfumo huo uwe na uwazi na uwajibikaji kwa shule zote.

Chama hicho pia kimependekeza kufanyike tathmini ya mgawanyo wa majukumu ya usimamizi wa elimu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, kikieleza kuwa mfumo huo unaweza kuleta mkanganyiko wa mamlaka, uratibu na uwajibikaji.

TPTU inapendekeza pia masuala ya utamaduni yarudishwe chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa hoja kwamba elimu na utamaduni vina uhusiano wa moja kwa moja katika kujenga utambulisho, maadili na historia ya Taifa.

Hoja nyingine ni kupanua wigo wa mamlaka ya Kamishna wa Elimu pamoja na kuundwa na kuimarishwa kwa Baraza la Ushauri la Elimu kama chombo cha kitaifa cha kutoa ushauri kuhusu sera, maendeleo na uendeshaji wa elimu.

TPTU pia inataka Serikali itoe mara kwa mara nyaraka rahisi zinazoeleza sheria za kazi, haki za wafanyakazi na wajibu wa waajiri, ili kupunguza migogoro inayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria.

Hoja zafika Bungeni

Baada ya kukosa mrejesho uliotarajiwa, TPTU ilipeleka hoja hizo Bungeni Aprili 6, 2024 kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. KM/TPTU/BUNGE/1/24.

Kwa mujibu wa chama hicho, Bunge lilipokea hoja hizo na Mei 24, 2024 likamwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. EB/20/90/01/108, likiomba changamoto hizo zishughulikiwe.

TPTU ilielekezwa kufuatilia suala hilo katika wizara hiyo.Hata hivyo, baada ya muda bila kupata mrejesho, chama hicho kilirudi tena Bungeni.

Juni 3, 2025, Bunge lilimwelekeza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kushughulikia changamoto hizo kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. JB.65/79/01/44.

Baadaye, Mei 12, 2026, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo aliwasilisha changamoto hizo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, kupitia barua yenye Kumbukumbu Na. FC.82/349/01.

TPTU inasema hatua hiyo imeifanya hoja hizo kufika katika eneo linalohusika zaidi na masuala ya kazi na ajira.

TPTU yasema haitaki malumbano

Katika taarifa yake, TPTU imesisitiza kuwa lengo lake si kuingia katika malumbano na Serikali, bali kupata mfumo wa majadiliano na utekelezaji unaowezesha changamoto hizo kutatuliwa.

Chama hicho kimesema hoja hizo zinagusa wizara na taasisi mbalimbali, zikiwemo elimu, kazi na ajira, uwekezaji, kodi, hifadhi ya jamii, afya, fedha, mitihani na utawala.

Kwa msingi huo, TPTU inataka Serikali iweke utaratibu wa pamoja wa kuzishughulikia badala ya kila taasisi kumwelekeza mdau kwenye taasisi nyingine.

Chama hicho kinataka kila hoja itolewe majibu rasmi, iwe imekubaliwa, imekataliwa, imehitaji marekebisho ya sheria au imepelekwa katika taasisi nyingine.

Wito kwa wamiliki wa shule

TPTU pia imewataka wamiliki na waajiri wa shule zisizo za serikali kuwachukulia walimu na wafanyakazi kama rasilimali muhimu katika utoaji wa elimu.

Chama hicho kinataka waajiri wazingatie sheria za kazi, watoe mikataba halali, walipe mishahara kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, wawasilishe michango ya hifadhi ya jamii na waheshimu haki za wafanyakazi.

Pia kimewataka waajiri kuweka mazingira salama na yenye heshima kazini na kushirikiana na TPTU katika kutatua migogoro kabla haijawa mikubwa.

Wito kwa walimu na wafanyakazi

Kwa upande wa walimu na wafanyakazi, TPTU imewataka kujifunza sheria, kutimiza wajibu wao, kulinda taaluma na kutumia njia halali za kudai haki pale wanapohisi wameonewa.

Chama hicho kimesisitiza kuwa kufanya kazi katika shule isiyo ya serikali hakupunguzi hadhi ya mwalimu wala kuondoa nafasi yake katika mfumo wa elimu wa Taifa.

Wanahitaji mrejesho na ufumbuzi

TPTU imesema haitaki kila hoja yake ikubaliwe bila mjadala, bali inataka Serikali isikilize, ijibu na kutoa sababu pale ambapo hoja fulani haiwezi kutekelezwa.

“Kama Serikali inaona hoja fulani haiwezi kutekelezwa, itueleze kwa nini. Kama inahitaji kubadilisha sheria, itueleze. Kama inahitaji muda, itueleze. Kama inahitaji wizara nyingine, iziratibu,” chama hicho kimesema.

Kwa mujibu wa TPTU, kinachohitajika sasa ni kuwepo kwa “mrejesho na ufumbuzi” baada ya mchakato wa zaidi ya miaka mitatu wa kuwasilisha na kufuatilia hoja hizo.

Chama hicho kimesema kinatambua hatua ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano ya kuthibitisha kupokea hoja hizo na kuendelea kuzifanyia kazi.

Hata hivyo, kimeomba mchakato huo uende kwa wakati na kwa uratibu wa Serikali nzima ili changamoto hizo zisitafsiriwe kuwa mzigo wa taasisi moja pekee.

TPTU imesisitiza kuwa, haidai kila pendekezo lake likubaliwe, bali inataka kuwepo kwa majibu rasmi na ushirikishwaji wa wadau katika hatua zinazofuata.

Kwa mtazamo wa chama hicho, hoja 27 si malalamiko pekee, bali ni ajenda inayolenga kuboresha mfumo wa elimu, ajira na uwekezaji nchini. "Tuliomba tangu 2023. Tumefuatilia hadi 2026. Sasa tunaomba mrejesho na hatua.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here