NA DIRAMAKINI
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Antonio Guterres ameonya kuwa, dunia inaingia katika kipindi hatarishi cha hali ya hewa kutokana na kuimarika kwa El Niño, hali ya asili ya tabianchi inayotarajiwa kufikia kilele kuelekea mwishoni mwa mwaka huu na mwanzoni mwa mwaka kesho.
Guterres amesema, kuongezeka kwa joto la bahari pamoja na mwenendo wa kupanda kwa wastani wa joto duniani ni viashiria vya hatari ya kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa katika maeneo mbalimbali ya sayari.
Onyo hilo limekuja wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO) likibainisha kuwa,El Niño imeendelea kuimarika na inatarajiwa kuwa na nguvu zaidi katika miezi ijayo, huku hali hiyo ikitarajiwa kuendelea hadi Februari,2027.
Kwa mujibu wa WMO, athari za El Niño katika mifumo ya joto na mvua zinaweza kuendelea kujitokeza hadi mwaka 2027, jambo linaloweza kuongeza hatari ya mafuriko, ukame na vipindi vya joto kali katika maeneo mbalimbali duniani.
Wataalamu wa tabianchi wanaeleza kuwa, El Niño ni hali ya asili inayohusishwa na ongezeko la joto la wastani la maji katika eneo la Mashariki na katikati ya Bahari ya Pasifiki ya Ikweta.
Hata hivyo, licha ya kutosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hali hiyo inaweza kuongeza zaidi joto na kuchochea matukio ya hali mbaya ya hewa katika dunia ambayo tayari inakabiliwa na ongezeko la joto kutokana na shughuli za binadamu, hususan uchomaji wa nishati za mafuta.
Bw.Guterres amesema,dunia kwa sasa iko katika mazingira ya hali ya hewa ambayo hayajawahi kushuhudiwa, akizitaka nchi kuongeza kasi ya kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha mikakati ya kulinda jamii dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.
Amesema,changamoto kubwa inayokabili dunia ni kuhakikisha kwamba kasi ya hatua zinazochukuliwa kuwalinda watu inaendana au kuzidi kasi ya kuongezeka kwa hatari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Tanzania katika tahadhari ya El Niño
Huku tahadhari hiyo ikiendelea kutolewa katika ngazi ya kimataifa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema, hali ya El Niño iliyoanza kujitokeza nchini tangu Aprili, 2026 imeendelea kuimarika na inatarajiwa kuwa na ushawishi mkubwa katika mwenendo wa mvua za msimu wa Vuli kati ya Oktoba na Desemba 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a amesema, kuimarika kwa El Niño kunaweza kuchagiza ongezeko la mvua katika maeneo ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki, huku pia kukiwa na uwezekano wa kutokea vipindi vya hali mbaya ya hewa katika baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa Dkt.Chang’a, hali hiyo inahitaji jamii, taasisi na mamlaka husika kuwa makini na taarifa za hali ya hewa ili kuchukua hatua stahiki kwa wakati, hasa katika maeneo yanayoweza kukumbwa na athari za mvua nyingi au matukio mengine ya hali mbaya ya hewa.
“Hali ya El Niño inatarajiwa kuendelea kuimarika na kufikia kiwango cha El Niño yenye nguvu kubwa kuelekea mwishoni mwa mwaka na hivyo kusababisha ongezeko la mvua katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Dkt. Chang’a.
Mwelekeo huo unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazohitaji kuendelea kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa, hususan wakati wa msimu wa Vuli unaotarajiwa kuanza Oktoba.
Kuongezeka kwa mvua kunaweza kuwa na manufaa kwa sekta zinazotegemea maji, ikiwemo kilimo na uzalishaji wa chakula, lakini pia kunaweza kuongeza hatari za mafuriko, uharibifu wa miundombinu, magonjwa yanayohusishwa na maji na athari nyingine endapo maandalizi hayatakuwa ya kutosha.
Aidha, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa taarifa sahihi na zinazotolewa kwa wakati, huku jamii ikihimizwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzitumia katika kufanya maamuzi yanayoweza kupunguza madhara.
Kwa upande wa mamlaka, kuimarika kwa mifumo ya tahadhari za mapema, maandalizi ya kukabiliana na majanga na ushirikiano kati ya wataalamu wa hali ya hewa, vyombo vya habari, serikali na jamii ni miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia kupunguza athari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
Hivyo, wakati El Niño ikiendelea kuimarika kimataifa na kutarajiwa kufikia nguvu kubwa kuelekea mwisho wa mwaka, Tanzania inakabiliwa na umuhimu wa kuongeza maandalizi na kuhakikisha utabiri wa hali ya hewa unawafikia wananchi kwa lugha inayoeleweka na kwa wakati unaofaa.
Tags
Angalizo kuhusu El Niño 2026
El Niño
Habari
Kimataifa
Maafa ya Mvua
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
