Rais Dkt.Samia ametoa Shilingi bilioni 13 kujenga Daraja la Loya,litaokoa maisha na kufungua fursa za kiuchumi Uyui-Profesa Shemdoe

TABORA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia Shilingi Bilioni 13 kutumika kujenga daraja la Loya linalounganisha kata za Loya na Miswaki wilayani Uyui pamoja na wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Amesema, ujenzi wa daraja hilo utasaidia kuimarisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo kwenda masokoni, kuongeza fursa za biashara kwa wananchi na muhimu zaidi, kuondoa changamoto ya wananchi kupoteza maisha na mali zao wanapovuka Mto Loya, hususan wakati wa mvua.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo Septemba 5, 2026, alipotembelea eneo la Mto Mhwala, unaofahamika pia kama Mto Loya, ambako daraja hilo linatarajiwa kujengwa katika eneo lenye jiografia ya ardhi oevu.

Amesema,ujenzi wa daraja hilo utakuwa suluhisho la muda mrefu kwa wananchi wa vijiji vya Loya, Miswaki, Isuli, Lutona, Mabeshi na Simbo-Igunga, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara, hali inayowaathiri katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Prof. Shemdoe amesema kati ya Shilingi Bilioni 13 zilizoidhinishwa, kiasi cha fedha zitatumika kumlipa Mhandisi Mshauri anayesimamia maandalizi ya michoro na kusimamia ujenzi kwa niaba ya Serikali, huku Shilingi Bilioni 10.4 zikitumika moja kwa moja katika ujenzi wa daraja hilo.

“Tumshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha na kuleta kiasi hicho cha Shilingi Bilioni 13 za ujenzi wa daraja la Loya, ambalo litaboresha biashara na usafirishaji wa mazao ya kilimo katika Kata za Loya na Miswaki wilayani Uyui pamoja na wilaya ya Igunga,” amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe amesema ujenzi wa daraja hilo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja baada ya kuanza kwa ujenzi, hatua ambayo itawaondolea wananchi gharama ya Shilingi 1,000 wanazolipa kwa kutumia kivuko kilichotengenezwa kwa juhudi za mwananchi aliyejitolea kujenga daraja la miti.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya ujenzi huo, Prof. Shemdoe amesema Mhandisi Mshauri anatarajiwa kukamilisha kazi ya usanifu mwezi Septemba 2026, na kwamba mwezi Oktoba Serikali itatangaza zabuni ya kumpata mkandarasi atakayetekeleza mradi huo.

Amesema,ujenzi rasmi unatarajiwa kuanza mwezi Desemba 2026 baada ya kusainiwa kwa mkataba, na utakamilika ndani ya mwaka mmoja, ifikapo Novemba 2027.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Igalula, Mhe. Juma Kawamba amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumtuma Prof. Shemdoe, ambaye amemtaja kuwa ni mchapakazi, kufikisha kwa wananchi habari njema ya ujenzi wa daraja la Loya.

Mhe. Kawamba amesema,wananchi wa eneo hilo wamepoteza ndugu zao wengi kutokana na changamoto ya kuvuka eneo hilo, hivyo ujenzi wa daraja hilo utakuwa faraja kubwa na hatua muhimu ya kulinda maisha na mali zao.

Ametoa wito kwa wananchi kuwapokea na kushirikiana vizuri na wakandarasi watakaotekeleza mradi huo, pamoja na kulinda vitendea kazi na miundombinu itakayojengwa ili iweze kudumu na kunufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Loya ni wa kimkakati kwa kuwa, ukikamilika, utarahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo, kufungua fursa za biashara, kupunguza gharama za usafiri na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya wananchi wa Loya, Miswaki wilayani Uyui na maeneo ya wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, sambamba na kulinda maisha na mali za wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here