NA DIRAMAKINI
BARAZA Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) limepitisha kwa wingi azimio linalolenga kuhamasisha mabadiliko katika namna Dunia inavyooneshwa kwenye ramani, hususan kuhusu ukubwa halisi wa Afrika na mabara mengine ambayo kwa muda mrefu yameonekana yakiwa makubwa au madogo kuliko uhalisia wake.
Azimio hilo linalojulikana kama “Correct the Map”, limepitishwa Ijumaa kwa kura 164 za kuunga mkono dhidi ya moja, huku nchi sita zikijizuia. Marekani ndiyo iliyokuwa nchi pekee iliyopiga kura kulikataa azimio hilo.
Azimio hilo liliwasilishwa na Togo kwa niaba ya nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa, linalojumuisha nchi zote 54 za bara hilo na lilipata pia uungwaji mkono kutoka kwa Umoja wa Afrika (AU).
Ingawa azimio hilo halina nguvu ya kisheria ya kuzilazimisha nchi au taasisi kubadili ramani wanazotumia, linahimiza matumizi mapana zaidi ya mifumo ya kuchora ramani inayowakilisha kwa usahihi zaidi uwiano wa ukubwa wa maeneo ya nchi na mabara duniani.
Moja ya mifumo inayopendekezwa ni Equal Earth, ambayo ina uwezo wa kuonesha ukubwa wa maeneo ya nchi na mabara kwa uwiano unaokaribia zaidi uhalisia, ingawa kufanya hivyo kunasababisha baadhi ya maumbo ya maeneo hayo kupotoshwa kwa kiwango fulani.
Akizungumza kabla ya kura, Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo, Robert Dussey amesema, ramani si michoro rahisi ya kijiografia, bali zina nafasi muhimu katika kuunda namna watu wanavyouelewa ulimwengu.
“Ramani huunda uelewa wetu wa dunia. Huongoza elimu, huchochea fikra na huathiri mitazamo ya pamoja,”amesema.
Waziri Dussey amesisitiza kuwa,ni wakati kwa Waafrika kuchukua jukumu la kuleta mabadiliko wanayoweza kuyafanya wenyewe.
“Ni wakati sasa sisi Bara la Afrika kuchukua jukumu la kubadili yale tunayoweza kuyabadilisha wenyewe,”amesema.
Mjadala huo umejikita zaidi katika matumizi ya Mercator Projection, mfumo wa kuchora ramani uliotengenezwa karne ya 16 na ambao umekuwa miongoni mwa mifumo inayotumiwa zaidi duniani.
Mfumo huo uliundwa mwaka 1569 na mchora ramani kutoka Flanders, Gerardus Mercator. Ingawa unahifadhi kwa kiasi kikubwa maumbo ya maeneo ya nchi na mabara, una kasoro kubwa katika kuonesha ukubwa wao halisi.
Kwa mfano, maeneo yaliyo karibu na ncha za Dunia yanaweza kuonekana kuwa makubwa zaidi kuliko ukubwa wake halisi.
Hali hiyo imekuwa ikifanya maeneo ya Kaskazini kama Greenland na sehemu za Ulaya kuonekana kwa ukubwa zaidi ikilinganishwa na maeneo ya karibu na Ikweta ikiwemo Afrika.
Aidha,wataalamu wa ramani wanaeleza kuwa, matumizi ya Mercator hayakuanzia katika lengo la kupotosha ukubwa wa mabara. Mfumo huo uliundwa hasa kwa ajili ya urambazaji wa baharini.
Faida yake kubwa ilikuwa kuwezesha mabaharia kupanga njia za safari kwa kutumia mistari iliyonyooka huku wakidumisha mwelekeo uleule wa dira. Kwa sababu hiyo, Mercator ikawa nyenzo muhimu kwa mabaharia, wavumbuzi na wasafiri wa baharini katika karne zilizofuata.
Hata hivyo, mfumo huo unapowekwa katika matumizi ya kielimu au kuonesha uwiano wa ukubwa wa mabara, unazua changamoto kwa sababu hauwakilishi kwa usahihi ukubwa halisi wa maeneo mbalimbali.
Kampeni ya Correct the Map inahimiza serikali, mashirika ya kimataifa na taasisi za elimu kuanza kutumia mifumo ya ramani inayozingatia zaidi uwiano wa ukubwa wa maeneo.
Miongoni mwa inayopendekezwa ni Equal Earth, iliyobuniwa mwaka 2018 na wachoraji ramani Tom Patterson, Bernhard Jenny na Bojan Šavrič.
Mfumo huo uliundwa kwa lengo la kutoa taswira inayowakilisha kwa uwiano sahihi zaidi ukubwa wa maeneo ya nchi na mabara duniani.
Tofauti yake kubwa na Mercator ni kwamba Equal Earth inalenga kuhifadhi zaidi uwiano wa eneo, badala ya kuhifadhi kikamilifu maumbo ya maeneo hayo. Kwa hiyo, baadhi ya maumbo yanaweza kuonekana yamepinda au kubadilika kwa kiasi, lakini ukubwa wake ukawakilishwa kwa usahihi zaidi.
Aidha,pamoja na kupata uungwaji mkono mkubwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, azimio hilo halilazimishi nchi wanachama kubadili mifumo ya ramani wanayotumia.
Badala yake, linatoa msukumo wa kisiasa na kielimu kwa serikali, taasisi za kimataifa na taasisi za elimu kutafakari upya mifumo inayotumika katika vitabu, madarasa, machapisho na nyenzo nyingine za kuelimisha umma kuhusu jiografia ya dunia.
Kwa upande wa Afrika, mjadala huo umepewa uzito kutokana na hoja kwamba namna bara hilo linavyooneshwa kwenye ramani inaweza kuathiri uelewa wa watu kuhusu ukubwa na nafasi yake katika jiografia ya dunia.
Pia,kupitia azimio hilo, waungaji mkono wa kampeni hiyo wanataka dunia iende zaidi ya swali la “ramani inaonekanaje?” na kuzingatia pia swali la “ramani inaonesha ukweli kwa kiwango gani?”.
Tags
Afrika
Azimio la Umoja wa Mataifa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Correct the Map
Habari
Kimataifa
Ramani ya Afrika
Umoja wa Mataifa (UN)
