GEITA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashiriki Maonesho ya 9 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita kuanzia tarehe 23 Septemba hadi 03 Oktoba,2026.
Katika maonesho haya, BoT inatoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa sera ya fedha na mchango wake katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha uchumi wa nchi, pamoja na namna ya kuwekeza katika dhamana za serikali za muda mfupi na muda mrefu.
Pia, elimu inatolewa kuhusu mifumo ya malipo ya taifa inayowezesha miamala kufanyika kwa haraka na usalama, sambamba na namna ambavyo BoT inasimamia sekta ya fedha ili kuhakikisha taasisi za kifedha zinafanya kazi kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria.
Vilevile, wananchi wanaelezwa kuhusu utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha pamoja na fursa za masomo zinazotolewa na Chuo cha BoT kwa wanaotaka kujijengea ujuzi katika masuala ya fedha na kibenki.
Aidha, BoT inatoa elimu maalumu kuhusu namna ya kutambua alama za usalama katika noti za Tanzania na njia sahihi za kutunza noti na sarafu ili kudumisha ubora na matumizi salama ya fedha taslimu.
Maonesho hayo yanaongozwa na kaulimbiu “MADINI NI UTAJIRI, TUWAJIBIKE KWA AMOJA KUFIKIA DIRA YA TAIFA 2050.”







