Uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma waahirishwa

NA DIRAMAKINI

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeujulisha umma wa Watanzania kuwa, hafla ya uzinduzi wa majengo ya wizara, taasisi za Serikali na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma iliyopangwa kufanyika Septemba 8,2026 imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.
Muonekano wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 7,2026 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) jijini Dodoma.

Taarifa hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tu, tangu Serikali kutangaza kukamilika kwa sehemu kubwa ya miundombinu ya eneo hilo na maandalizi ya uzinduzi rasmi wa majengo ya wizara,taasisi za Serikali na mtandao wa barabara za lami ambao umekamilika.

Septemba 6,2026 jijini Dodoma, Waziri wa wizara hiyo,Profesa Palamagamba Kabudi alisema, kukamilika kwa Mji wa Serikali Mtumba ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu yenye miundombinu inayokidhi mahitaji ya shughuli za Serikali za kisasa.

“Kukamilika kwa majengo hayo kutatoa mazingira ya kisasa ya kufanyia kazi kwa jumla ya watumishi 18,510, hatua inayoonesha ukubwa wa uwekezaji uliofanyika na nafasi ya Mji wa Serikali katika kuboresha mazingira ya utendaji wa Serikali,”amesema.

Prof.Kabudi alisema, mji huo haukujengwa kwa siku moja na kwamba Safari yake ilianza mwaka 2018, wakati Serikali ilipoanza kutekeleza hatua za awali za kujenga mazingira ya kuwezesha Wizara na taasisi za Serikali kufanya kazi Dodoma.

Hatua ya kwanza ya ujenzi ilianza Novemba 28, 2018, kwa kujenga majengo 23 ya muda kwa ajili ya ofisi za Serikali. Majengo hayo yalikamilika Machi 22, 2019, na kuwezesha baadhi ya Wizara na taasisi kuanza kuhamia eneo hilo.

Katika hatua hiyo pia zilijengwa ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na jengo la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), hatua iliyoweka msingi wa kuanza kwa shughuli za Serikali Mtumba wakati maandalizi ya ujenzi wa majengo ya kudumu yakiendelea.

“Huo ukawa mwanzo wa safari ya kuligeuza eneo la Mtumba kutoka eneo la ujenzi wa majengo ya Serikali na kuwa mji maalumu wenye mifumo ya barabara, maji, umeme, mawasiliano, TEHAMA, usalama na huduma nyingine muhimu,”amesisitiza.

Kuhusu awamu ya pili alisema,hatua kubwa zaidi ilifikiwa Oktoba 2021, Serikali ilipoanza awamu ya pili ya ujenzi iliyolenga kujenga majengo ya kudumu kwa ajili ya Wizara na taasisi mbalimbali.

“Tofauti na awamu ya kwanza iliyolenga kuweka mazingira ya awali ya kuanza kwa shughuli za Serikali, awamu ya pili imehusisha ujenzi wa miundombinu ya kudumu na mifumo mbalimbali inayolenga kuufanya Mji wa Serikali kuwa eneo kamili la shughuli za Serikali,”alisema.

Hata hivyo, huenda hafla hiyo imeahirishwa kutokana na Taifa kupata msiba ambapo mume wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mheshimiwa Hafidh Ameir Hassan amefariki dunia leo Septemba 7, 2026 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa Tanzania,Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, Hafidh alikuwa akitibiwa ugonjwa wa moyo na alifariki dunia majira ya saa mbili asubuhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here