Huduma jumuishi za fedha zaing'arisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Kimataifa

PORT MORESBY-Benki Kuu ya TaTanzania (BoT) imetambuliwa miongoni mwa taasisi tatu bora kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (Alliance for Financial Inclusion-AFI) duniani, kutokana na uongozi madhubuti katika sera za huduma jumuishi za fedha na juhudi za kupunguza pengo la kijinsia katika upatikanaji wa huduma za fedha.
Utambuzi huo ulitolewa kupitia vipengele mbalimbali vya tuzo na vyeti vya AFI, ikiwemo Tuzo ya Azimio la Maya (Maya Declaration Award), inayotambua mafanikio ya nchi katika kuweka, kupima na kutekeleza ahadi za kuendeleza huduma jumuishi za fedha.

Benki Kuu pia ilitambuliwa kwa nafasi yake katika utekelezaji wa Mpango Kazi wa Denarau (Denarau Action Plan), ambao unaweka msisitizo katika kuendeleza huduma jumuishi za fedha kwa wanawake na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza pengo la kijinsia katika huduma za fedha.

Aidha, Benki ilitambuliwa kwa juhudi za kuandaa na kutekeleza sera mbalimbali zinazochangia kupunguza pengo hilo.

Vyeti hivyo vya utambuzi vilipokelewa na Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati wa Jukwaa la Kimataifa la Sera za Huduma Jumuishi za Fedha la mwaka 2026, lililofanyika Port Moresby, Papua New Guinea, kuanzia tarehe 1 hadi 4 Septemba 2026.

Akizungumza katika mjadala uliobeba mada kuhusu “Afya ya Kifedha: Msingi wa Uchumi Himilivu na Mustakabali Jumuishi.”, Gavana Tutuba alieleza uzoefu na maendeleo ya Tanzania katika kuimarisha afya ya kifedha kupitia mfumo unganishi wa malipo ya kidijitali, sera na mikakati ya maendeleo ya sekta ya fedha, pamoja na programu za elimu na uwezo wa kifedha.

Aidha, alisisitiza kuwa upatikanaji wa huduma za fedha ni hatua ya mwanzo, na kwamba matokeo halisi yanapaswa kuonekana katika uwezo wa wananchi kusimamia mapato na matumizi yao, kuweka akiba, kutumia mikopo kwa tija, kukabiliana na misukosuko ya kifedha na kuboresha maisha yao.

Pia, Gavana Tutuba alipewa heshima ya kukabidhi Tuzo ya Ubunifu katika Huduma Jumuishi za Fedha ya Nestor Espenilla Jr. ya mwaka 2026 kwa Benki Kuu ya Zambia, iliyotwaa tuzo hiyo.

Jukwaa hilo liliandaliwa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI), inayojumuisha taasisi wanachama kutoka nchi 84, na lilihudhuriwa na zaidi ya washiriki 700 kutoka nchi 79.
Mafanikio hayo yanaakisi hatua zinazotekelezwa na Benki Kuu katika kuimarisha mazingira ya kisera na kiudhibiti, kukuza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za fedha, kupunguza pengo la kijinsia na kuhakikisha huduma rasmi za fedha zinawafikia na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.

Pia yanaonesha maendeleo ya Tanzania katika kutekeleza ahadi za Azimio la Maya, linalohimiza taasisi wanachama wa AFI kuweka na kutekeleza malengo mahsusi na yanayopimika ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma jumuishi za fedha, pamoja na kupunguza pengo la kijinsia.

Katika hatua nyingine, Meneja wa Idara ya Huduma Jumuishi za Fedha, Bi. Nangi Massawe, alitunukiwa cheti cha utambuzi katika kipengele cha Uongozi wa Sera za Huduma Jumuishi za Fedha, huku Meneja wa Idara ya Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha, Dkt. Khadijah Kishimba, akitambuliwa katika kipengele cha Mwenendo wa Soko na Uwezeshaji wa Watumiaji wa Huduma za Fedha.

Vilevile, watumishi watatu wa Benki Kuu, Bw. Sadiki Nyanzowa, Bw. Thomas Mongella na Bi. Kidee Mshiriri, walihitimu Programu ya Uongozi katika Huduma Jumuishi za Fedha ya Fletcher School na kutunukiwa vyeti vya kuhitimu.
Mafanikio hayo yanaongeza uwezo wa wataalamu wa Benki Kuu katika kuongoza uandaaji na utekelezaji wa sera na mikakati ya huduma jumuishi za fedha.

Jukwaa hilo lililoongozwa na kaulimbiu ya “Uchumi Himilivu, Mustakabali Jumuishi”, liliwakutanisha Magavana na Naibu Magavana wa Benki Kuu, viongozi wa mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha, taasisi za maendeleo, sekta binafsi, watoa huduma za teknolojia na washirika wengine kutoka nchi mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here